Na Pamela Mollel,Mirerani
Serikali imefanikisha kufunga mfumo wa Kamera za CCTV zipatazo 306 kuzunguka ukuta wa mgodi wa madini ya Tanzanite ulipo katika mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro, mkoani Manyara.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila wakati akipokea mradi huo wenye thamani ya sh, bilioni 1.2 uliotekelezwa na kampuni ya Starfix Enterprises .
Prof Msabila alisema kuwa mradi huo unalenga kuimarisha usalama eneo tengefu la machimbo ya madini ya Tanzanite ,kupitia Mfumo wa Usalama wa CCTV Camera ,ambavyo vinafanya kazi nyakati zote za mvua, vumbi,usiku na baridi .
Ametoa rai kwa wadau wote wa sekta ya madini katika eneo hilo tengefu la Mirerani kujiepusha kabisa na vitendo vya rushwa na utoroshaji wa madini.
Aidha Profesa Msanjila amesema mwezi February ,2019 Wizara ilialika makampuni sita kwa ajili ya kushiriki zabuni ya usambazaji na ufungaji wa mfumo wa kamera wa usalama katika ukuta wa migodi ya Tanzanite Mirerani ambapo wazabuni 5 waliwasilisha gharama zao.
" Makampuni na watu mbalimbali walikuja wizarani na wengine waliletwa na taasisi za serikali kwa lengo la kutaka kupatiwa tenda ya kufunga mfumo wa CCTV kamera katika eneo hili la Mirerani, gharama walizowasilishwa zilikua kubwa sana, kwa mfano wapo waliowasilisha gharama ya sh.bil. 83, bil. 76, bil.33, na wengine bil. 27 lakini kama Wizara tulichambua na kuona gharama hizo kuwa ni kubwa sana na kuamua kutowapatia kazi, ndipo tulipoipatia kazi kampuni ya Starfix Enterprises kwa gharama ya sh. Bil.1.2 " alisema Profesa Msanjila.
Katika hatua nyingine ,Prof,Msanjila alisema kuwa wizara yake imekamilisha ujenzi wa jengo la wafanyabiashara wa madini ( Brokers House ) , jengo la kituo cha pamoja ( One Stop Centre ) ndani ya ukuta wa Mirerani na kwamba uwekaji wa miundombinu ya umeme na taa kuzunguka ukuta umekamilika.
"Ufungaji wa kamera za ulinzi ( CCTV ) kuzunguka eneo la ukuta wa migodi ya Tanzanite umekamilika na leo hii tumepokea mradi huo vilevile ujenzi wa jengo la Scanner, ufungaji wa scanner na kuweka mfumo wa Biometric entrace unatarajia kuanza muda si mrefu, na utagharimu takribani kiasi cha sh. bil. 4.2."Alisema katibu
Hata hivyo alisema ujenzi wa miundombinu hiyo, mapato ya serikali yameongezeka kabla ya ujenzi kutoka sh.mil.238 kwa mwaka 2016 - 2017 hadi kufikia sh. bil. 3.587 kwa mwaka 2018 - 2019 ambapo miundombinu hiyo imewezesha kupatikana mawe ya Tanzanite kutoka katika mgodi wa Saniniu Laizer ambayo yalivunja rekodi ya uzito duniani wa kilo 9.27, 5.103 na 6.33 yenye jumla ya thamani ya sh.bil. 12.590,689,974.94 huku serikali ikijipatia mapato ya sh.mil. 919,120,368.17 kutoka malipo ya mrahaba, ada ya ukaguzi na ushuru.
Naye Katibu Mkuu wizara ya ulinzi Dkt Faraji Kasidi alisema kuwa mfumo huo utasaidia maafisa na Askari waliopewa jukumu la kuimarisha ulinzi katika ukuta wote wa mirerani kutekeleza kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa
Aidha alitaja manufaa yanayotarajiwa hupatikana baada ya kufungwa kwa kamera hizo ni pamoja na kukuza pato la taifa kutokana na uthibiti wa utoroshwaji wa madini uliokuwa ukifanywa na watu wasiokuwa waaminifu kabla ya kujenga ukuta
Katibu Mkuu wizara ya madini Profesa Simon Msanjila akikabidhi mfumo wa kamera za CCTV kwa Katibu Mkuu Wizara ya Uliñzi Dkt Faraji Kasidi leo Mkoani Manyara
Katibu Mkuu Wizara ya Uliñzi Dkt Faraji Kasidi akikabidhi mfumo wa kamera wa CCTV kwa jeshi la ulinzi leo Mkoani Manyara
Katibu Mkuu Wizara ya Madini,Profesa Simon Msanjila akizungumza katika hafla ya mradi wa CCTV leo Mkoani Manyara.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment