Na Grace Gurisha
MTENDAJI MKuu wa Taasisi inayohusisha na michezo kwa watu wenye ulemavu wa akili (Special Olympics Tanzania, Charles Rays amesema jamii inatakiwa itambue kuwa watoto wenye ulemavu wa akili na wao wanahaki ya kucheza michezo mbalimbali mashuleni kama watoto wengine.
Rays amesema hayo leo Novemba 17,2020 mkoani Mwanza katika mafunzo ya walimu wa shule za msingi, makocha, maofisa elimu maalumu, maofisa michezo kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya Special Olympics.
Amesema katika kufanikisha mradi wa Stavros Niarchos Foundation ( SNF) wenye dhima ya kuleta ukaribu wa kujifunza na wa kucheza miongoni mwa watoto wenye ulemavu wa akili na wasio na ulemavu mashuleni, lengo ni kuleta ushirikishi wa walemavu katika nyanja zote.
Rays amesema pia, lengo lingine ni pamoja na kuielezea jamii kupitia michezo kuwa walemavu wanaweza kushirikiana na wanajamii wengine katika masuala ya kijamii bila kujali ulemavu wao.
"Special OlympicsTanzania tunaendelea kusimamia maandalizi ya mashindano kati ya shule na shule, baadae kufikia ngazi ya mkoa katika shule mbalimbali zilizopo nchini Tanzania," amesema Rays
Amesema mafunzo hayo yamefika kwa siku mbili Novemba 16 na 17,2020 kwenye ukumbi wa Kanisa la Anglican Mtakatifu Nicholas Wilaya ya Nyamagana, Kata ya Nyamagana, ambapo washiriki walikuwa 76.
Mkurugenzi huyo, amesema walimu walikuwa 40, makocha 26, maofisa elimu maalumu wa wilaya tano na maofisa michezo wa wilaya tano, ambapo Wilaya zilizotoa washiriki ni Wilaya ya Nyamagana, Ilemela, Misungwi, Mwanza Juju na Sengerema .
Rays ambae ndiyo alikuwa mkufunzi aliyeongoza mafunzo hayo, amesema Mradi wa SNF katika awamu ya pili ya utekelezaji umelenga kuzifikia shule takribani 85 kutoka Mkoa wa Morogoro, Dar es Salaam, Tanga, Mtwara na Mwanza.
Kwa upande wa Mwalimu Mkuu wa Michezo kutoka Shule ya Msingi, Semi, Zacharia Leonard amesema mafunzo waliyoyapata yamewasaidia kuwatambua watoto wenye ulemavu wa akili kuwa ni sehemu ya jamii na watu ambao wakipewa nafasi wanafanya vizuri.
"Nimepokea mafunzo haya kwa namna ya pekee kwa sababu ni mafunzo ambayo ni jumuishi hata watoto ambao wanamahitaji maalumu ni kundi la watoto na watu wazima ambao mahala pengi wamesahaulika na kuonekana kuwa ni duni," amesema Mwalimu Leonard
Naye, Mwalimu wa Elimu Maalumu, Lilian John kutoka Shule ya Msingi, Nyamalango amesema wamejifunza mambo mengi ikiwa ni pamoja na jinsi ya kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalumu na wale ambao ni wakawaida katika masula ya michezo mashuleni.
"Kupitia mafunzo haya nimejua namna ya kuwapanga watoto wenye mahitaji na ambao hawana, lakini pia tumepata kitu kipya zaidi cha kuwachanganya watoto hawa katika michezo ili wawaone kama watoto wengine wa kawaida,"
" Dhana hii tumeipata kupitia mafunzo haya, kwa hiyo tumeongeza maarifa mengine ndani ya ile tuliyokuwa nayo ya kuhusiana na elimu maalumu, "amesema Mwalimu John
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya Special Olympics Tanzania wakionesha vyeti vyao walivyokabidhiwa baada ya kumaliza mafunzo ya jinsi wa kuwasaidia watoto kwenye mahitaji maalumu.
Mtendaji Mkuu wa Special Olympics Tanzania, Charles Rays akitoa mafunzo kwa washiriki 76 kutoka Shule mbalimbali zilizopo kwenye Wilaya tano za Mkoa wa Mwanza.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment