***********************************
Jonas Kamaleki, Dodoma
Tangu Rais John Pombe Magufuli aingie madarakani miaka mitano iliyopita mambo makubwa na ya kuishangaza Dunia yamekuwa yakifanyika. Hivi karibuni Tanzania imefanya uchaguzi kwa kutumia fedha za ndani (Tshs. Bilioni 262) bila kuwategemea wafadhili.
Jambo hili ambalo lilionekana kama haliwezekani kwa baadhi ya watu wenye mawazo mgando, limewezekana na kuwaacha watu vinywa wazi. Heko Rais Magufuli kwa ubunifu na uthubutu wako.
Rais wa Tanzania, John Magufuli anasema katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, 2020 Serikali ilitenga Sh331 bilioni lakini Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetumia Sh262 bilioni.
Kwa miongo zaidi ya mitano nchi hii imekuwa ikiwategemea wafadhili kwa kiwango kikubwa ili kuendesha mipango yake ya uchumi. Ikumbukwe kuwa katika Azimio la Arusha, Falsafa ya Mwalimu Nyerere ya Ujamaa na Kujitegemea ndiyo ilipaswa kuwa msingi au dira ya uchumi wa Tanzania.
Ni jambo la kupongezwa kuona nchi inarudi kwenye msingi huo. Tunaona miradi mikubwa ya maendeleo inaendeshwa tena kwa ubora kwa kutumia fedha za ndani yaani za walipa kodi. Mradi wa ujenzi wa Reli ya kiwango cha kimataifa (SGR) unajengwa kwa fedha za ndani zaidi ya trilioni 6 fedha za Kitanzania, Mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere unaogharimu takriban shilingi trilioni 6.55 unaendelea kwa fedha ya mlipakodi na miradi mingine ya afya, elimu na maji.
Tanzania imepanda viwango vya kimataifa na kujulikana karibu dunia nzima kwa hatua hasa za kukuza uchumi ambazo Rais Magufuli amekuwa akizichukua. Kutoka kwenye nchi maskini na kuingia uchumi wa kati kabla ya 2025 ni jambo ambalo limewashangaza watu wengi.
Akizindua Bunge la 12 Rais Magufuli alibainisha juhudi mbalimbali za Serikali katika kukuza uchumi na kuibadilisha Tanzania kutoka kwenye uchumi tegemezi na kuingia kwenye uchumi wa kujitegemea.
“Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, tulijitahidi kusimamia vizuri uchumi wetu, ambapo ulikua kwa wastani wa asilimia 7 kwa mwaka. Aidha, Pato ghafi la Taifa limeongezeka kutoka shilingi trilioni 94.349 mwaka 2015 hadi kufikia shilingi trilioni 139.9 mwaka 2019”, alisema Rais Magufuli.
Mfumuko wa bei ulidhibitiwa kutoka asilimia 6.1 mwaka 2015 hadi kufikia wastani wa asilimia 4.4 na kuongeza akiba ya fedha ya kigeni kutoka Dola za Marekani bilioni 4.4 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 5.2 mwezi Julai, 2020 ambazo zinaiwezesha nchi kununua bidhaa na huduma kwa miezi 6.
“Zaidi ya hapo, kwenye miaka mitano iliyopita, tuliongeza mauzo yetu ya nje kutoka Dola za Marekani bilioni 8.9 mwaka 2015 hadi Dola za Marekani bilioni 9.7 mwaka 2019; na pia kuvutia uwekezaji wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 14.6, sawa na zaidi ya shilingi trilioni 30”, alisisitiza Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli alisema kuwa Serikali ilipunguza umasikini wa kipato hadi kufikia asilimia 26.4 kwa takwimu za mwaka 2017/2018. Mafanikio haya, bila shaka, ndiyo yamewezesha, mwezi Julai 2020, nchi yetu kutangazwa kuingia kundi la nchi za uchumi wa kati kutoka kundi la nchi masikini. Na mafanikio hayo yamepatikana miaka mitano kabla ya muda uliopangwa, yaani mwaka 2025.
Hivi karibuni wakati wa hafla ya kuapishwa kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa tumemsikia Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango ambaye naye aliapishwa siku hiyo akisisitiza kukuksanya mapato kwa kiwango kikubwa na kusisitiza kuwa fursa zipo za kupata fedha hapa nchini.
Rais Magufuli amesikika mara kadha akisema, Nchi hii ni TAJIRI NA SI MASKINI. Watu wenye fikra duni hawamuelewi wanadhani anajisemea tu. Mimi namuunga mkono kwani anachosema ni ukweli usiopingika.
Unajiitaje maskini wakati una amani ambayo ni bidhaa adimu katika nchi nyingi. Una madini ya kila aina, almasi, dhahabu, chuma, shaba, tanzanite ambayo inapatikana Tanzania pekee Duniani. Una gesi, mafuta , bahari, maziwa, mito, mabonde, mbuga za wanyama, Mlima Kilimanjaro na sehemu za kihistoria kama vile Bagamoyo, Kilwa na Zanzibar, halafu unasema sisi ni maskini. Hiyo kama si laana ni nini.
Mikataba kandamizi ya madini iliyokuwa inadidimiza nchi kiuchumi imefumuliwa na nchi kuanza kupata mabilioni ya fedha. Baada ya mgogoro uliodumu tangu mwaka 2017, Kampuni ya Barrick na Serikali zimeunda kampuni ya Twiga itakayosimamia migodi mitatu iliyokuwa chini ya kampuni ya Acacia.
Kwenye kampuni hiyo mpya, Barrick itamiliki asilimia 84 ya hisa zote huku Serikali ikiwa na asilimia 16. Utaratibu huo ni utekelezaji wa sheria mpya ya madini iliyopitishwa mwaka 2017.
Ikumbukwe kuwa hivi karibuni Mhe. Rais John Pombe Magufuli alipokea gawio la Shilingi bilioni 100 kutoka kampuni ya Twiga inayomilikiwa kwa ubia na Serikali ya Tanzania na Barrick. Kiasi hicho cha fedha kinaweza kujenga vituo vya afya 250 kwa gharama ya milioni 400 kila kituo. Hili ni jambo la kujivunia kwa taifa.
Ununuzi wa ndege 11 kwa kulipa keshi ni ubunifu mwingine wa Jemedari, Dkt. John Pombe Magufuli. Ndege hizi zimetoa mchango mkubwa hususan katika mlipuko wa COVID 19 kwa kuwanusuru watanzania waliokuwa wamekwama katika nchi mbalimbali baada ya mataifa husika kuzuia usafiri wa anga.
Umeme umesambazwa kwenye vijiji zaidi ya elfu 9 na kubakiza vijiji vichache ambavyo vitasambaziwa umeme mapema katika kipindi cha pili cha Serikali ya Awamu ya Tano.
Haya yote yamefanyika kwa kipindi kifupi cha Serikali ya Awamu ya Tano kutokana na ubunifu na uthubutu wa Rais Magufuli na timu yake. Ni ukweli usiopingika kuwa uongozi wa Jemadari Magufuli ni mfano wa kuigwa na umeshangaza wengi ndani na nje ya nchi.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment