VIJANA HAWANA HAJA YA KULALAMIKA AJIRA KWA SABABU MAZINGIRA RAFIKI YA KUJIAJIRI YAPO | Tarimo Blog

 Na Grace Gurisha


MKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya Jenga Afya Tokomeza Umaskini (Jatu PLC), Peter Isare amesema vijana hawana haja ya kulalamikia ajira kwa sababu tayari kuna mazingira rafiki ambayo wanaweza kujiajiri wenyewe na kuleta mabadiliko.

Aidha, Kampuni hiyo kwa mara ya kwanza inaingiza hisa zake sokoni Novemba 23,2020 katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DCE) kwa Sh. 420 kwa hisa moja.

Isare amesema hayo leo Novemba 13,2020 katika Ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa mwaka wa wanahisa na wawekezaji wa Kampuni hiyo, ambapo walipokea taarifa ya maendeleo.

Amesema kikubwa ni kwamba vijana waangalie namna gani ya kushirikiana na kuaminiana kama Kampuni za kitanzania, kwa sababu wanaweza kushirikiana kwa pamoja katika suala la kulima kwa pamoja.

"Vijana tusidhani kwamba kilimo kinachozungumziwa na Jatu ni kile cha mtu kuamka asubuhi na kwenda shambani, tunachokimaanisha ni kwamba tunaweza kushirikiana kwa kilimo cha pamoja,

" Tunaweza kutumia miundombinu mikubwa ya kisasa na machine za kisasa, ambapo tunaweza kujenga kiwanda kikubwa, kijana anakuwa muwekezaji, wanaweza kutengeneza ajira na pengine wanaweza kuwalisha wengine, "amesema Isare

Akizungumzia suala la Hisa, Mkurugenzi huyo amesema tangu mwaka 2016 walikuwa na mchakato wa kuingia katika soko la  hisa, ambapo rasmi wamepata kibali hicho, lengo ni kuhakikisha kwamba watanzania wengi wanapata umiliki wa Kampuni hiyo.

" Kikubwa tunataka kuboresha viwanda ili viweze kuzalisha kwa kiasi kikubwa ili soko letu la ndani na nje liweze kukuwa, hivyo tunahitaji kukuza mtaji wetu na njia rahisi ni kupitia soko la  hisa la Dar es Salaam,

"Tayari tumeshaweka misingi na utaratibu nzuri ambao ni rahisi kuingia, tunawaomba watanzania wajitokeze kwa wingi kununua hisa hizo ili waweze kupata mtaji wa kutosha wa kuendeleza miradi mikubwa," amesema Isare

Isare amesema Jatu ni Kampuni ya kitanzania inayohusiana na masuala ya kilimo, ambapo wamejikita katika masoko, viwanda na kilimo kwa lengo la kuinua uchumi wa viwanda hapa nchini.

Kwa upande wake, Mjumbe wa bodi ya kampuni hiyo, Emanuela Kaganda amesema Jatu ni Kampuni ya kwanza ya Tanzania ya kilimo kwenda kwenye soko la  hisa, ambapo hakuna Kampuni nyingine ya kilimo ambayo imeingia kwenye soko hilo.

"Tunaamini kwamba itakwenda kufanya vizuri sana kuliko Kampuni zingine kutokana na bidhaa tunazozipeleka sokoni. Tumeona Kampuni za  vinywaji hasa bia zinafanya vizuri kwa kuangalia hilo, hii Kampuni ya chakula itafanya vizuri zaidi," amesema Kaganda

Naye, Meneja wa Jatu Sacco's, Ester Kihuya amesema kuwa wanalima kilimo cha kisasa, kwa hiyo wananchi wasiogope kuwekeza, zamani walikuwa wanapata hasara ya kulima kwa sababu hakukuwa na wataalamu hats wakupima udongo.

"Ni waondoe hofu huku kunawataalamu wa kutosha na nyenzo za kilimo za kisasa, hata kama mvua ikinyesha na maji yamejaa shambani  kuna kifaa cha ambacho kinaweza kulima ndani ya maji, " amesema Kihuya .

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Jenga Afya Tokomeza Umaskini (JATU PLC),  Peter Isare akizungumza na waandishi habari (hawapo pichani), katika mkutano wa mwaka wa Kampuni hiyo uliyofanyika jijini Dar es Salaam, ukihusisha wanahisa na wawekezaji.
Mjumbe wa Bodi ya JATU PLC, Emanuela Kaganda akizungumza katika mkutano wa mwaka wa Kampuni hiyo kuhusiana na mikakati ya kujenga viwanda vingi hapa nchini
 Wanahisa na Wawekezaji katika Kampuni ya JATU PLC wakiwa katika mkutano wa mwisho wa mwaka wa Kampuni hiyo, ambapo walipokea taarifa za maendeleo.



Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2