HOSPITALI YA SANITAS YAPEWA SIKU SABA KUKAMILISHA MALIMBIKIZO YA MISHAHARA KWA WATUMISHI WAKE | Tarimo Blog








 NAIBU Waziri Wizara ya  Kazi, Ajira na Vijana Mhe.Patrobas Katambi ameiagiza hospitali ya Sanitas ya jijini Dar es Salaam kuhakikisha wanalipa malimbikizo ya mishahara kwa wafanyakazi wao, rai hiyo ameitoa leo mara baada ya kuzuru ofisini hapo kwa lengo la kujiridhisha na masuala ya kisera yanayohusiana na ajira, kazi na vijana.

Akiwa ofisini hapo, Naibu waziri amebaini watumishi wa Hospitali hiyo kutokupatiwa stahiki zao za kiutumishi ikiwemo mishahara yao kwa kipindi cha miezi 13 sasa kwa kigezo cha kuyumba biashara kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Corona.

 Katambi amesema  kulipa mishahara watumishi ni takwa la kikatiba na haliwezi kuvunjwa kwa kigezo chochote kile, hasa ikizingatiwa kaulimbiu ya wizara kwa awamu hii ni "Mtumishi alipwe ujira wake  kabla jasho halijakauka." Lengo likiwa kuhakikisha kwamba mfanyakazi mtanzania anapata haki yake kwa wakati na kulinda ajira za wazawa.

"Watumishi hawa wan amahitaji binafsi, wanafamilia zinawategemea na wanatakiwa kulipa Kodi za serikali kupitia mishahara yao, kitendo cha ninyi kutowapa mishahara yao kipindi chote hiki sio tuu kuwakoseshea mahitaji yao ya msingi bali mnakwamisha pia Kodi za serikali." Ameongeza Naibu Waziri.

Aidha  Naibu  Waziri huyo ameutaka uongozi wa Sanitas kuwapa mikataba isio na ukomo watumishi wanaostahili mikataba hiyo, kuwa na vyama vya wafanyakazi,  kuwasilisha nyaraka zinazohusu umiliki wa kampuni ili ziweze kupitiwa upya pia Uongozi uwe na  sera mbalimbali hususan ya ajira na UKIMWI Ili ziweze kufuatwa kikamilifu katika majukumu ya kiutawala.

Kwa upande wake kamishna wa Ajira Nchini  Tanzania Brigedia Mbindi  amesema ziara hii ni endelevu kwa nchi nzima lengo likiwa ni kuhakikisha sheria na  miongozo mbalimbali ya kazi inafuatwa kikamilifu na wafanyakazi wanafanya kazi katika mazingira bora.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe Daniel Chongolo amesema Kinondoni inaendelea kutatua  changamoto mbalimbali zinazowakabili waajiriwa wa sekta binafsi  hivyo kwa ziara hii kutapunguza changamoto kwa waajiriwa na kuwapa mazingira mazuri wawekezaji katika kutimiza majukumu yao.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri amepongeza uongozi wa kiwanda cha coca-cola kwanza kwa kufuata kikamilifu sheria za kazi hususan Katika kuwapa kipaumbele wafanyakazi wazawa na kuwapatia mafunzo wazawa Katika yale maeneo ya utaalamu.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri ametembelea Hospitali ya Sanitas iliyopo Mikocheni na Kiwanda cha coca-cola kwanza.



Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2