Na Mwandishi wetu, Globu ya Jamii
JESHI la Polisi hapa nchini limesema kuwa hali ya ulinzi na Usalama wa Nchi imeendelea kuwa shwari kutokana na kazi kubwa inayofanywa na Jeshi hilo kwa kushirikiana na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama, pia Jeshi limepata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi wapenda amani au raia wema ambao wamekuwa wakitoa taarifa za uhalifu pamoja wahalifu kwa Jeshi la Polisi nchini.
Katika Taarifa iliyotelewa na Kamishna wa Operesheni Na Mafunzo, Liberatus Sabas (CP) imesema kuwa licha kuwepo na hali ya utulivu lakini yapo matukio machache ambayo yamejitokeza ambayo ni tofauti na matukio ya kipindi cha nyuma.
Matukio hayo ni kama vile, Unyang’anyi wa kutumia silaha, Mauaji, Ajali za barabarani, Shule kuungua moto, Wanafunzi kuacha masomo na kujiunga na makundi ya kihalifu.
Imeeleza taarifa hiyo kuwa,Unyang’anyi wa kutumia silaha.(Ujambazi) Jeshi la Polisi kwa mwaka huu limefanikiwa kupunguza makosa ya ujambazi wa kutumia silaha kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma na mwaka jana kuanzia mwezi Januari hadi Novemba (2019) kulikuwa na makosa 378 huku mwaka huu kuanzia Januari hadi Novemba (2020) yamepatikana makosa 273 ya kutumia silaha hii ikiwa ni tofauti ya makosa 105 sawa na asilimia 27%.
Kwa Upande wa Mauaji imeelezwa kuwa Kwa kiasi kikubwa mauaji yanayotokea kwa sasa nchini ni wivu wa mapenzi na wananchi kujichukulia sheria mkononi kutokana na hali hiyo Jeshi la Polisi limefanikiwa kutoa elimu kwa wananchi kutokujichukulia sheria mkononi huku likiwataka viongozi wa dini kuingilia kati katika kutoa elimu ili kusaidia kupunguza mauaji yatokanayo na wivu wa mapenzi kwani wengi ni waumini wa madhebu yao na wanawasikiliza sana.
Kwa upande wa ajali za Barabarani kwa mwaka 2019 na 2020 ni kama ifuatavyo, Januari hadi Novemba 2019 matukio ya ajali yalikuwa 2722, ajali zilizosababisha vifo ni 1117, waliofariki dunia ni 1329 huku majeruhi wakiwa 2717. Huku mwaka huu kuanzia Januari hadi Novemba 2020 matukio ya ajali 1800, ajali za vifo 935, waliofariki dunia 1158 na majeruhi 2089, huku kukiwa na utofauti wa matukio ya ajali 922 sawa na 33.9%, ajali za vifo 182 sawa na 16.3%, waliokufa 171 sawa na 12.9% na waliojeruhiwa 628 sawa na 23.1%.
Matukio ya Shule kuungua moto taarifa hiyo imesema kuwa Miongoni mwa matukio yalioshika kasi na nafasi kubwa mwaka huu ilikuwa ni kuungua kwa majengo ya Shule na hii imetokana na sababu tofauti ambazo ni Hitilafu za Umeme, Migogoro Mashuleni na Uzembe, huku shule za watu Binafsi/Taasisi za Kidini zikiwa jumla 20 na za Kiserikali zikiwa ni 11 hii inakamilisha jumla ya shule 31 zilizoungua toka Januari mpaka Novemba mwaka huu.
Wanafunzi kuacha masomo na kujiunga na makundi ya kihalifu, Jeshi la Polisi nchini linawaomba wazazi na walezi kufuatilia nyendo za watoto wao kwani kumekuwa na wimbi kubwa la watoto kuacha shule na kwenda kujiunga na makundi ya kihalifu, miongoni mwa waalifu hao ni wale waliokuwa Kibiti na hatimae baada ya kupigwa na Jeshi la Polisi kwa kushilikiana na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama walikimbilia nchi jirani ya Msumbiji, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo CP Liberatus Sabas amesema hadi sasa wapo wanafunzi waliokuwa wameacha shule na kujiunga na vikundi vya kihalifu ambao wamekamatwa wakiwa wanavuka kuelekea nchini Msumbiji na wengine tayari wameishafanikiwa kuvuka kuingia nchini humo.
Aidha Kamishna CP Sabas licha ya kuwataka wazazi kuwalinda na kufuatilia mienendo ya watoto wao amewataka wananchi kuchukua tahadhali wakati huu wa kuelekea Sikukuu za mwisho wa mwaka kwani Jeshi la Polisi kwa kushilikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama wamejipanga kikamilifu kukabiliana na uhalifu.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment