MCHELE ULIOHARIBIKA WATEKETEZWA ZANZIBAR | Tarimo Blog


Wafanyakazi wa Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) wakishusha tani 52 za mchele ulioharibika kwa ajili ya kuuangamiza katika Jaa la Kibele, Mkoa wa Kusini Unguja.
Sehemu ya Vipolo vya mchele ulioharibika ukiwa umezongwa na wadudu katika jaa la Kibele Mkoa wa Kusini Unguja
Mkurugenzi Idara za Huduma za Maabara wa Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar Nadir Khatib Hassan akizungumza na wandishi wa habari kuhusu kuangamizwa mchele ulioharibika katika Jaa la Kibele.

(Picha na Makame Mshenga.)

Na Ramadhani Ali,  MAELEZO

WAKALA wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) imeteketeza tani 52 za mchele ulioingizwa nchini na Mfanyabiashara Suleiman Abdalla mwezi Machi mwaka jana ukiwa umeshaharibika na haufai kwa matumizi ya binadamu.


Mchele huo ambao ulikuwa umo kwenye makontena mawili bandarini Malindi, ulitakiwa urejeshwe ulikonunuliwa ama uangamizwe kwa gharama za mfanyabiashara mwenyewe ambaye alikubali kugharamia zoezi la kuuangamiza.


Mkurugenzi Idara za Huduma za Maabara wa Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar Nadir Khatib Hassan, ambae alisimamia uangamizaji  huo katika jaa la Kibele, alisema uliingizwa nchini tarehe 15.3.2019 kutoka Pakistan.


Alisema mchele huo ulikosa ubora kwa matumizi ya binadamu na ulikuwa na wadudu wengi tokea ulipoingizwa nchini.


Aliwashauri wafanyabiashara kuwa waangalifu wanapokwenda kununua bidhaa nje na kufuatilia kwa karibu taratibu zote za usafirishaji ili kujiepusha na gharama zisizokuwa za lazima.


Hivi karibuni Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdalla alifanya ziara katika bandari ya Malindi na kugundua uwepo wa kontena mbili zilizosheheni mchele huo mbovu na akatoa muda wa siku tatu kuondoshwa makontena hayo kwa kufuata taratibu za kiafya.


Alionya vikali kwamba Serikali haitosita kumfutia kibalia mfanyabiashara yeyote atakayejihusisha na kuingiza bidhaa zilizopitwa na muda wa matumizi ama zilizokuwa hazina viwango.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2