Muonekano wa Jengo la Utawala la Kituo cha TAFIRI-SOTA-Rorya baada ya Ujenzi mpya kukamilika kutokana ruzuku iliyotolewa na serikali kupitia COSTECH
Mkuu wa kituo cha TARIRI-SOTA, Bi Tausi Khitentya akifafanua kuhusu utendaji kazi wa kituo hicho baada ya kkamilika kwa majengo yaliyojengwa kwa ruzuku kutoka serikalini kupitia COSTECH.
Mwakilishi wa kikundi cha Mcheo akiongea afisa kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH)
MIAKA minane baada ya kuanzishwa kwa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) 1980, mradi wa kusimamia na kuratibu masuala yanayohusu sangara ulianzishwa katika Kijiji cha Sota wilayani Rorya, mkoani Mara mwaka 1988. Mradi huo ulipokamilika, shughuli zake zikaendelezwa kama kituo kidogo cha TAFIRI.
Wakati unaanzishwa, mradi ulichimba mabwawa tisa ambayo bado yapo mpaka leo yakitumika kufundishia wafugaji, kuzalisha vifaranga na kufanikisha utafiti wa samaki. Mwaka 2004 kituo kilianzisha teknolojia ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba na mwaka 2007 wananchi wakaanza kufundishwa teknolojia hiyo ambayo sasa wanaitumia kufuga samaki kwenye ziwa Victoria.
Mpaka Machi mwaka huu, TAFIRI Sota haikuwa na majengo ya ofisi hivyo kulazimika kupanga kwenye nyumba za watu binafsi. Mwaka 2018 kituo hicho kidogo kiliomba ufadhili wa kiasi cha shilingi milioni 532.1 kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kijengewe jengo la kuangulia vifaranga, jengo la utawala pamoja na maabara ya utafiti.
Tayari majengo mawili yamekamilika na kuanza kutumika tangu Machi mwaka 2020 hivyo kukipunguzia kituo hicho gharama za uendeshaji na kutoa utulivu wa akili kwa wafanyakazi 12 wanaokihudumia kituo hicho kwa sasa.
Kwa sasa, majengo ya maabara na utawala yamekamilika ingawa hayana vifaa muhimu. Jengo la utawala linatumia samani za zamani ambazo hata hivyo hazikidhi mahitaji huku maabara ikikosa vifaa muhimu kupimia sampuli ili kupata matokeo ya utafiti au uchunguzi uliokusudiwa.
Ikipata vifaa vinavyohitajika, maabara hii inatarajiwa kupima ubora wa chakula cha samaki, magonjwa ya samaki, udongo, maji, mifumo ya samaki wenyewe na mimeamaji huku jengo la utawala likifanikisha shughuli nyingine muhimu.
Mkuu wa Kituo cha TAFIRI Sota, Tausi Khitentya anasema majengo hayo mawili yamewaondolea kero nyingi na kuwaongezea ari ya kufanya kazi kwani sasa ni rahisi kwao kupatikana kwa kuwa wananchi wanajua zilipo ofisi zao. Hata hivyo, anaiomba Serikali na wadau wengine kuendelea kusaidia kuboresha miundombinu inayohitajika ili kuongeza tija zaidi ya ufugaji samaki kanda ya ziwa na nchini kwa ujumla.
Licha ya jengo la kutotoreshea vifaranga, Bi Tausi anasema wanauhitaji wa nyumba za wafanyakazi na kibanda cha mlinzi.
Jengo la maabara limekamilika na lipo tayari kufanya kazi wakati huo lile la utawala likiwa linatumika hivi sasa hivyo kuinufaisha taasisi, wafanyakazi wake, wafugaji na wadau wengine wa samaki.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment