Mtafiti kiongozi wa mradi wa kuzalisha migomba kwa njia ya maabara akionesha atua mbalimbali wanazopitia katika uzalishaji.
Kituo cha Tengeru kilicho chini ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) iliyoanzishwa mwaka 2016, kimejielekeza kuwasaidia wakulima wa mbogamboga, maua na matunda. Kwa kushirikiana na mamlaka nyingine pamoja na wadau wa kilimo, kituo hicho kimejipanga vya kutosha kutoa mbegu bora za migomba.
Ingawa uzalishaji wa mbegu hizo ulianza siku nyingi, Kituo cha Tengeru kupitia TARI kiliomba ruzuku ya kiasi cha shilingi Milioni 400 kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ili kujenga maabara itakayoiongezea uwezo wa kuzalisha miche mingi zaidi hivyo kukidhi mahitaji ya wateja ilionao.
Uzalishaji wa mbegu hizo za migomba unatokana na ukweli kwamba ekari moja inahitaji miche 444 ambayo kwa njia ya kawaida ya kung’oa machipukizi kutoka kwenye mashamba yaliyopo na kwenda kuyapandikiza katika shamba jipya haiwezi kukidhi mahitaji.
Kwa kutumia teknolojia ambayo huuongezea mmea uwezo wa kujitengenezea chakula mpaka saa 16 badala ya nane za kawaida, maabara hii iliyofadhiliwa na COSTECH, imeweza kukuzwa migomba kwa haraka hivyo kuweza kupandikizwa shambani ndani ya muda mfupi.
Ofisa utafiti wa Tari Tengeru, Bi Grace Kindimba anasema kufanikisha hilo wanatumia teknolojia ya tissue culture ambayo huwataka kuweka miche ya migomba katika mwanga wenye kati ya lux 3,000 mpaka 3,600 hivyo kufanikisha uzalishaji wa migomba 15,000 kila baada ya miezi minne na kumwezesha mkulima kuwa na migomba yenye ukubwa sawa, isiyo na magonjwa na itakayozaa kwa wakati mmoja naye kuwa na ratiba ya kuvuna ndizi na kuzipeleka sokoni.
Maabara ya kuzalisha miche ya migomba kwa teknolojia ya tissue culture ilianza uzalishaji mwaka 2009 na mpaka mwaka 2018, ilikuwa inazalisha wastani wa miche 2,000 kwa kila miezi minne ingawa uwezo wake wa mwisho ilikuwa miche 5,000. Kuanzia Oktoba 2018, maabara hiyo ilianza kufanyiwa ukarabati ili kuiboresha na kuiongezea uwezo. Mradi huo ulipaswa kukamilika Juni 2020 lakini janga la ugonjwa wa homa ya mapafu inayosabanishwa na virusi vya Corona (Covid – 19) lilichelewesha ukamilikaji wake.
Wakati Wakala ya Ujenzi wa Nyumba Tanzania (TBA) ikitarajiwa kukamilisha sehemu chache zilizobaki, mzabuni anatarajiwa kuingiza na kuvifunga vifaa vinavyotakiwa kuanzia mwishoni mwa Oktoba 2020.
Itakapokamilika na kuendelea kufanya kazi kwa uwezo mkubwa zaidi, licha ya migomba, maabara hii pia itazalisha miche ya viazi mviringo na wakati huo, utaratibu wa kuzalisha miche ya vanilla, minanasi na viazi vitamu ukiendelea
Tayari maabara inao uzoefu wa kufanya kazi hivyo kuwanufaisha walengwa wanaojumuisha wafanyakazi wa taasisi hiyo, wanafunzi wa vyuo vikuu, wakulima pamoja na wajasirimali.Ukiacha wataalamu wa Tari Tengeru ambao watapata sehemu ya kutekeleza majukumu yanayolingana na taaluma walizonazo kwa ukubwa zaidi, itaongeza kasi ya utafiti wa kuzalisha mbegu bora za mbogamboga, matunda na viungo vya chakula (spicies).
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment