TBA KUWACHUKULIA HATUA KALI WADAIWA SUGU WA KODI ZA MAJENGO | Tarimo Blog


Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo nchini (TBA,) Mbunifu Majengo. Daud Kondoro akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na hatua za kisheria zitakazochukuliwa dhidi ya wadaiwa sugu wa kodi za nyumba na majengo yanayosimamiwa na Wakala hiyo, leo jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) mbunifu Majengo  Daud Kondoro (katikati) akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na hatua za kisheria zitakazochukuliwa dhidi ya wadaiwa sugu wa madeni ya nyumba na majengo, kulia ni Mkurugenzi wa idara ya miliki wakala hiyo (TBA,)  Said Mndeme, leo jijini Dar es Salaam.


Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA,) imesema kuwa hadi sasa jumla ya fedha zipatazo shilingi bilioni nne zinadaiwa kwa wapangaji  zikiwemo taasisi za umma zinazotumia nyumba hizo zinazosimamiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA.)

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mtendaji Mkuu wa TBA, Mbunifu Majengo Daud Kondoro amesema kuwa wapangaji wote zikiwemo taasisi za umma zinatakiwa kuhakikisha wanalipa madeni hadi kufikia mwisho wa mwezi huu, baada ya hapo hatua kali zitachukuliwa ikiwemo wapangaji kuondolewa kwenye nyumba hizo.

"Kwa sasa TBA imeazimia kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wapangaji wote tunaowadai, moja ya hatua zitakazochukuliwa ni kuwaondoa wadaiwa sugu kwa nguvu kwa kutumia dalali wa Mahakama ambao wamepewa zabuni hiyo kwa niaba ya TBA...Tuna Kampuni mbili za udalali wa Mahakama ambazo ni Yono Auction Mart na Ms.Harvest Tanzania Limited na tayari wamekabidhiwa orodha ya wadaiwa wote kwa hatua zinazofuata na zoezi hili litafanyika katika Mikoa yote nchini." Ameeleza Kondoro.

Aidha amesema, katika hatua nyingine ya kuhakikisha fedha hizo zinalipwa ni kuwafungulia mashtaka wadai wote watakaoondolewa katika nyumba na majengo hayo.

Vilevile amewataka watumiaji wengine wa nyumba na majengo yanayosimamiwa na TBA kuendelea kulipa kodi zao kwa wakati ili kuepuka usumbufu wa aina yoyote.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa idara ya miliki (TBA,)  Said Mndeme amesema taasisi za Serikali zipatazo 17 zinadaiwa huku makusanyo ya madeni hayo yakielekezwa katika  kusaidia kufanya ukarabati wa baadhi ya nyumba na makazi.

Amesema, TBA imerahisha kufanya malipo kwa wateja wao na sasa malipo hayo yanafanywa kwa njia ya simu na kusema kuwa wataendelea kufanya marekebisho ya nyumba zote katika kila Halmashauri nchini.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2