TEHAMA ITUMIKE KATIKA KUONGEZA KASI YA UKUAJI WA UCHUMI-MAJALIWA | Tarimo Blog

Waziri wa Mawasiliano na Teknollojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile akimkaribisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, mgeni rasmi kwenye hafla ya utoaji tuzo kwa washindi wa mashindano ya TEHAMA ambapo Tanzania imeshika nafasi ya pili kidunia na ya kwanza Afrika. Tuzo hizo zimetolewa Dar es Salaam

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wananchi kutumia vizuri Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwenye shughuli za uzalishaji mali na utoaji huduma katika sekta mbalimbali ili kusaidia kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini pamoja na kuongeza ajira.


Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali imedhamiria kufikisha miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwenye maeneo mengi zaidi kwa lengo la kuongeza matumizi ya mawasiliano ya kasi (broadband) kutoka asilimia 45 ya sasa hadi asilimia 80 ifikapo mwaka 2025.

 

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Desemba 23, 2020) katika hafla ya utoaji tuzo kwa washindi mashindano ya TEHAMA yaliyoandaliwa na kampuni ya HUAWEI ambapo Tanzania imeshika nafasi ya pili kidunia na ya kwanza kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahala na Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwapongeza washindi na waandaaji wa mashindano hayo. Hafla hiyo imefanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

 

Waziri Mkuu amesema ili kufikia malengo hayo, Serikali itatoa kipaumbele kwenye masuala ya tafiti na ubunifu sanjari na kutambua na kusajili wataalamu wote wa TEHAMA nchini. “Vilevile, tutaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo HUAWEI katika kuhakikisha tunaanzisha vituo vya umahiri vya sayansi na teknolojia kwenye taasisi za elimu ya juu nchini kwa kuzingatia maeneo ya kimkakati katika kujenga uchumi imara na endlevu sambamba na kudhibiti athari hasi zinazoweza kutokea kutokana na matumizi ya TEHAMA.”

 

Wakati akizindua Bunge la 12 jijini Dodoma, tarehe 13 Novemba 2020, Rais Dkt. John Pombe Magufuli alisisitiza kuwa katika kipindi hiki ambacho dunia ipo kwenye mageuzi ya viwanda yanayoongozwa na sekta ya mawasiliano, Tanzania hainabudi kuendana na kasi ya kukua kwa sekta hiyo.

 

Pia, Waziri Mkuu amezitaka kampuni za ndani zinajishughulisha na masuala ya TEHAMA ziige mfano wa kampuni ya HUAWEI kwa kuwekeza zaidi kwa kundi la vijana kwa nia ya kuibua na kuendelea vipaji.

 

“Serikali kwa upande wake, itaendelea kutekeleza maelekezo ya Ilani ya uchaguzi ya CCM kwa mwaka 2020 ya kuimarisha na kuhamasisha matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika Uchumi wa kidijitali (yaani digital economy). Maeneo yatakayolengwa ni pamoja na Serikali mtandao, miundombinu ya TEHAMA katika nyanja zote za uchumi sambamba na kuimarisha ulinzi wa mitandao.”

 

Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa wito kwa washiriki na wale waliobahatika kushinda, kwamba wanatakiwa watumie vema fursa na uzoefu walioupata kupitia mashindano hayo na kuwa mfano wa kuigwa kwa wengine.


“Niwapongeze pia HUAWEI kwa mchango wao mkubwa katika kuimarisha uchumi wa Tanzania kupitia matumizi ya TEHAMA na huduma za kidijitali. Tukiendelea hivi na kwa kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi, tutakuwa katika nafasi nzuri ya kwenda sambamba na ukuaji wa matumizi ya TEHAMA.”


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2