Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
*TRC yawaomba wananchi kulinda miundombinu ya reli
SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC) kwa kushirikiana na Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki Hamis Taletale maarufu kama 'Babu Tale' wameanza mchakato wa kukarabati barabara ya Ngerengere iliyokuwa kero kwa wananchi kwa zaidi zaidi ya miaka 15.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC,) Mkuu wa kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano wa TRC Jamila Mbarouk amesema, TRC kwa kushirikiana na mkandarasi anayejenga reli ya kisasa wameshiriki kwa kutoa msaada huo kwa jamii baada ya Mbunge Taletale kuwafuata na kuwaeleza changamoto zinazowakabili wananchi wa Morogoro Kusini Mashariki.
"Tunaelewa kuwa reli ya kisasa inajengwa kwa kodi za watanzania na mradi huu lazima itunzwe na kuthaminiwa na wana Ngerengere na Watanzania kwa ujumla, na tutaendelea kushiriki katika kusaidia jamii kama Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Magufuli inavyosimamia katika kuhakikisha mtanzania anavyofanya shughuli zake kwa amani... Wana Ngerengere mmepitiwa na mradi huu wa reli ya kisasa niwahakikishie mapema mwakani mtakuwa wa kwanza kunufaika na mradi huu" Amesema.
Amesema, TRC kwa kushirikiana na Yepi Merkezi itachonga na kushindilia barabara hiyo kwa kilomita 60.54 zilizobaki na wataendelea kutekeleza na kushiriki katika miradi hiyo kwa jamii kama walivyoaminiwa na Serikali.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo hilo Hamis Taletale amesema, ukarabati wa barabara hiyo katika tarafa ya Ngerengere ni moja ya ahadi aliyoihaidi jimboni humo.
"Katika kampeni zangu nilihaidi kukarabati barabara hii, niliwahaidi wana Ngerengere hawatopanda malori tena nimeanza kazi katika barabara hii ambayo haijawahi kupitiwa na katapila kwa miaka 15 na tutafanya mengi zaidi katika Jimbo hili." Amesema.
Mbunge Taletale amesema atafanya kazi kwa spidi katika kuboresha sekta za Mawasiliano, afya na elimu kama Serikali ya awamu ya tano ilivyodhamiria.
"Huu ni mwanzo tuu nitatembea kwa speed katika kuilinda ilani ya Chama cha Mapinduzi, na tutaendelea kushirikiana na wakazi wa Ngerengere katika kuyafikia Maendeleo...Na ndani ya miaka hii mitano nitahakikisha ninajenga ofisi ya chama kwa kila kata ikiwa ni pamoja na usafiri." Amesema.
Kuhusiana na suala la elimu, Mbunge huyo amesema kuwa ameshawashirikisha wadau wa sanaa hasa wasanii wakiwemo Diamond Platnumz, Ali Kiba, Rayvanny na Mbosso ambao watachangia madawati ili wananfunzi waweze kusoma vizuri na kusema kuwa kero ya mtando katika eneo la Ngerengere litakoma ndani ya miezi mitatu ijayo.
Akimwakilisha Meneja TARURA wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Gebo Mlangwa amesema, barabara hiyo ni moja ya barabara 84 za Wilaya hiyo na katika tarafa ya Ngerengere tayari wamekarabati kilomita 10 kwa kiwango cha changarawe kwa gharama ya shilingi milioni 200 fedha za maendeleo zilizotolewa na Serikali.
Amesema, TRC wameanza kazi hiyo waliyohaidi jana na tayari wamechonga kilomita 3 na watachukua wiki tatu kukamilisha barabara hiyo.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment