Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
TAASISI zinazohusika na utekelezaji wa Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish) wamekutana kujadili na kufanya tathimini ya utekelezaji wa mradi huo wa miaka sita (6) ili kupima mafanikio na mapungufu yaliyojitokeza kabla ya kufanya maamuzi ya kuendelea na awamu ya pili ya utekelezaji wake.
Akitoa taarifa fupi ya utekelezaji wa Mradi huo kwa wadau waliohudhuria kikao hicho kwa njia ya mawasiliano ya kimtandao (Web conference) kutokea jijini Dodoma Disemba 16, 2020, Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah alisema kuwa kikao hicho cha tathimini ni moja ya taratatibu walizoziweka kuwa kila baada ya miezi sita timu ya wataalamu kutoka taasisi za utekelezaji pamoja na wafadhili wa mradi huo Benki ya Dunia wanakaa pamoja kutathimini maendeleo ya mradi huo ili kusaidia kusukuma utekelezaji pale ambapo pataonekana kuna mkwamo.
“Kwa ujumla niseme tangu mradi huu uanze hatujawahi kupata taarifa isiyoridhisha kutoka kwa wafadhili wa mradi, wamefurahishwa na utekelezaji unavyoendelea kwenye maeneo yote ikiwemo matumizi ya pesa, na ujenzi wa majengo mbalimbali na inatupa faraja kuona kwamba tunatekeleza mradi huu kama tulivyokubaliana,” alisema Dkt. Tamatamah.
Dkt. Tamatamah alisema kuwa wameshawasilisha ombi kwa Wizara ya Fedha kuongeza muda wa utekelezaji wa Mradi huo kwa mwaka mmoja zaidi badala ya kuisha mwaka 2021 uendelee mpaka 2022 ili kufidia mapungufu yaliyojitokeza kufuatia athari za mlipuko wa ugonjwa wa Korona ulioikumba Dunia mwanzoni mwa mwaka huu huku akisema Benki ya Dunia imeridhia ongezeko hilo la muda ili mradi huo uweze kutimiza adhma yake.
Aliendelea kusema kuwa kufuatia vikwazo vya kusafiri vilivyoweka katika baadhi ya maeneo ya nchi duniani kutokana na maradhi ya Korona wameamua kufanya vikao kupitia mawasiliano ya kimtandao na vikao hivyo vilianza tangu Disemba 14, 2020 ambapo wadau wamekuwa wakikutana kujadili maendeleo ya mradi huo na Disemba 18, 2020 ndio ilikuwa hitimisho kwa wadau wote kupitia taarifa ya utekelezaji na kukubaliana mambo ya msingi ya kufanya kabla kuendelea na utekelezaji kwa muda ulioongezwa.
Aidha, Dkt. Tamatamah aliongeza kwa kusema kuwa Benki ya Dunia imeahidi kuisaidia Tanzania kufanikisha mpango wake wa kutekeleza agenda yake ya uchumi wa Bluu huku akisema kuwa Wizara ipo tayari kuendelea kushirikiana na Benki hiyo katika kulinda rasilimali za uvuvi na kuleta maendeleo ya sekta ya uvuvi kwa ujumla.
Taasisi zinazotekeleza mradi huo ni Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya Tanzania Bara, Wizara Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi na Mamlaka ya Usimamizi wa Bahari Kuu zote kutoka Zanzibar.
Mradi huo wa SWIOFish tangu uanze kazi mwaka 2015 umekuwa ukitekeleza shughuli mbalimbali zinazohamasisha ulinzi wa rasilimali za bahari ikiwemo usafi wa fukwe za bahari, ujenzi wa majengo ya ulinzi shirikishi wa rasilimali za bahari (BMU) pamoja na ununuzi wa vifaa mbalimbali kama vile Boti ambazo zimesaidia kukomesha uvuvi haramu katika maeneo mbalimbali na kusaidia kutoa huduma kwa watalii nchini.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment