Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WATAALAMU wa Chuo cha cha Kumbukumbu cha Hubert Kairuki (HKMU,) wamefanya utafiti na kutoa machapisho kuhusu njia mpya ya kutibu malaria na magonjwa yanayowakumba watoto wanaozaliwa kabla ya wakati.
Hayo yamesemwa leo Desemba 16, 2020 jijini Dar es Salaam na Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Charles Mgone wakati wa mahafali ya 18 ya chuo hicho yaliyofanyika chuoni hapo.
Kwenye mahafali hayo, wahitimu 146 walitunukiwa stashahada ya uuguzi, 53 shahada ya uuguzi, 183 shahada ya udaktari wa binadamu na wawili shahada ya uzamivu ya udaktari wa binadamu.
Profesa Mgone amesema tafiti mbalimbali zinaendelea kufanywa na wanataaluma wa chuo na wanafunzi wake wa ngazi zote zingine zikihusu magonjwa ya kuambukizwa na yale yasiyo ya kuambukizwa.
Amesema katika mwaka huu wa 2020 baadhi ya wataalaamu wa chuo hicho wametoa machapisho kadhaa katika majarida ya kisayansi yakiwemo ya uchambuzi yakinifu kuhusu elimu ya uuguzi na ukunga nchini na utafiti kuhusu njia mpya za kutibu maralia.
Ameyataja machapisho mengine kuwa ni kuhusu uhusiano kati ya ugonjwa wa seli mundu na malaria, dalili za mwanzo za kuelekea kupata ugonjwa wa kisukari na aina ya magonjwa yanayowasibu watoto wachanga waliozaliwa kabla ya wakati.
Kadhalika amesema HKMU kimeendelea na mpango wake wa kufadhili masomo ya wafanyakazi wake kwa ngazi ya uzamili na uzamivu ndani na nje ya nchi.
Amesema wahadhiri wanne wamemaliza mafunzo yao ya uzamili hivi karibuni akiwemo Dk. Fulgence Mpenda, Dk. Jane Nyandele, Dk. Hosiana Msechu na Dk. Zahra Moraweji.
Profesa Mgone ameaema kwa sasa chuo hicho kina wahadhiri 15 wanaosomea shahada ya uzamivu na saba shahada ya uzamili katika fani mbalimbali huku wahadhiri sita wakipandishwa vyeo katika fani mbalimbali.
Amesema katika kuboresha ufundishaji chuo kimeajiri wafanyakazi wapya ili kuendana na ongezeko la wanafunzi na tangu Desemba 2019 mpaka Novemba mwaka huu chuo kimeajiri wafanyakazi wapya nane.
“Kwa niaba ya chuo napenda kuwapongeza wanataaluma na wanafunzi wote kwa hayo machapisho ambayo yametambulika kitaifa na kimataifa,” alisema
Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Afya na Elimu la Kairuki, Kokushubila Kairuki aliwapongeza wafanyakazi wote wa chuo hicho kwa namna wanavyozidi kukipandisha hadhi mwaka hadi mwaka kutokana na kila mmoja kuwajibika kwa upande wake.
“Kipekee napenda kumpongeza Profesa Mgone kwa umahiri na ubunifu wake uliohakikisha chuo hiki kinaendelea hata wakati wa janga la korona wakati wenzetu wanafunga vyuo yeye alihakikkisha hapa kila kitu kinakwenda sawa,” alisema
Aidha, ameipongeza Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kwa namna ambavo imekuwa ikitoa mchango wa kuhakikisha chuo kinapata anafunzi kwa kutangaza kozi zake kila yanapotokea maonyesho ya vyuo vikuu yanayoandaliwa na taasisi hiyo kila mwaka.
“Mbali na hilo TCU inazingatia sana ubora wa elimu nawapongeza sana na baraza la ufundi NECTA wamekuwa wakitupa ushirikiano mkubwa sana hasa kwenye shule yetu ya uuguzi ya Kairuku, wizara na serikali kwa ujumla wanatusaidia,” alisema Kokushubila.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment