YA UNGUJA YANABAMBA | Tarimo Blog

 




1. Ya Unguja yanabamba,

Hiyo raha hadi Pemba,
Wote sasa ni wajomba,
Kusiwepo kusutana.

2. Tulikuwa tunaomba,
Kutoka kwake Muumba,
Vile alivyotuumba,
Kusiwepo kusutana.

3. Wa mjini hata shamba,
Hata mji kule Fumba,
Tulitaka ile nyumba,
Kusiwepo kusutana.

4. Uchaguzi tuliyumba,
Na kuchafuliwa pamba,
Sote sasa tuko chemba,
Kusiwepo kusutana.

5. Wapo tuliowasomba,
Kwamba mjini watamba,
Sasa hata wale njemba,
Kusiwepo kusutana.

6. Mkuu wimbo kaimba,
Aina ya kwake nyumba,
Ili asiweze yumba,
Kusiwepo kusutana.

7. Mkwara waliuchimba,
Na maneno wakagomba,
Wakatulizana chemba,
Kusiwepo kusutana.

8. Mungu katupa Zanzibar,
Unguja ongeza Pemba,
Nchi moja tunatamba,
Kusiwepo kusutana.

9. Hussein hajawa mwamba,
Peke yake akitamba,
Kaka yake kamuomba,
Kusiwepo kusutana.

10. Maalim kule chemba,
Akailegeza kamba,
Ili Unguja na Pemba,
Kusiwepo kusutana.

11. Muda wa nyimbo kuimba,
Na barabara kuchimba,
Tuicheze hata samba,
Kusiwepo kusutana.

12. Pamoja tujenge nyumba,
Kwa fito kutoka shamba,
Msingi tukiuchimba,
Kusiwepo kusutana.

13. Twawahongera Zanzibar,
Hebu fukiza uvumba,
Acha tusakate rumba,
Kusiwepo kusutana.

14. Mwinyi, Maalim tamba,
Na Hemed jenga nyumba,
Visiwani kuwe bomba,
Kusiwepo kusutana.

15. Chini chini kuna myamba,
Kufika hapa twatamba,
Wamefanya vema kwamba,
Kusiwepo kusutana.

16. Vyama viwili sambamba,
Vimejitoa kimwamba,
Wameziacha kasumba,
Kusiwepo kusutana.

17. Zitto tusipomuimba,
Tutakuwa ni wa shamba,
Kaongoza kule chemba,
Kusiwepo kusutana.

18. Chama kichanga chatamba,
Makamu ndani ya nyumba,
Dume wameshalilamba,
Kusiwepo kusutana.

19. Magufuli naye mwamba,
Na mkali kama simba,
Hili wala hajayumba,
Kusiwepo kusutana.

20. CCM ingetamba,
Pekee kujenga nyumba,
Uamuzi wao bomba,
Kusiwepo kusutana.

21. Viongozi ni miamba,
Wanataka jenga nyumba,
Wa Unguja na Pemba,
Kusiwepo kusutana.

22. Wananchi wa Zanzibar,
Sasa wao ni miamba,
Watoke wacheze samba,
Kusiwepo kusutana.

23. Vidonda vilivyovimba,
Na maneno ya kugomba,
Yote tujifunge pamba,
Kusiwepo kusutana.

24. Tuombe kwake Muumba,
Kusitokee kizimba,
Tuweze kujenga nyumba,
Kusiwepo kusutana.

25. Sitini na nne imba,
Mapinduzi yalitamba,
Waafrika kwenye dimba,
Kusiwepo kusutana.

26. Tukukatae kuyumba,
Tunajenga moja nyumba,
Tuzikate kamba kamba,
Kusiwepo kusutana.

27. Tarehe nane Disemba,
Jumanne tunatamba,
Kata kata tunaimba,
Kusiwepo kusutana.




Na Lwaga Mwambande (KimpaB)

8/12/2020

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2