Afisa Tarafa Itiso iliyopo Wilaya ya Chamwino Remidius Emmanuel amegeuka mbogo na kumtaka Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwiyendaje iliyopo Kata ya Haneti Frank Kimbindu kujieleza na kutoa sababu zilizopelekea kusuasua kwa ujenzi wa vyumba viwili vya Madarasa kupitia fedha za mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R ) tangu fedha hizo zilipotolewa na Serikali Juni 2020 na matumizi yake kuanza mapema Mwezi Agosti, 2020.
Afisa Tarafa amehoji mbele ya kikao chake kilichohusisha Serikali ya Kijiji cha Mwiyendaje, Kamati ya Shule, Kamati ya Ujenzi na viongozi wa kata ya Haneti akiwa ziarani shuleni hapo huku akimtaka Mkuu wa Shule hiyo kueleza ni kwa nini licha ya Serikali kutoa fedha zote Milioni 40 lakini hadi leo bado ujenzi huo uko hatua ya msingi tena ndo wanaendelea kujaza kifusi kwenye msingi na kumtaka aeleze nani amekwamisha ujenzi huo wakati fedha zipo ?
"Hii haingii akilini kabisa, yaani Serikali imetoa fedha za ujenzi kwa aslilimia 100, wenzako mfano Shule ya msingi Dabalo ndani ya Tarafa hii wao walisha kamilisha ujenzi huu tangu Mwezi Desemba, 2020 nyinyi leo hata jamvi bado? Sasa nahitaji uandike maelezo ya kina unifahamishe na kujieleza sababu zipi ambazo zimetufikisha hapa na ueleze nani anatakiwa kuwajibika katika hili" Remidius Afisa Tarafa Itiso.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu huyo amesema kilichopelekea kusuasua kwa mradi huo ni kutokana na taratibu za mfumo wa kifedha pamoja na kupanda kwa bei ya Saruji bei iliyotofautiana na mchanganuo wa gharama za ujenzi (BOQ) na hivyo kusubiri bei ishuke, hata hivyo maelezo hayo yamepingwa vikali na Afisa Tarafa huku Mwalimu huyo akishindwa kujibu pale alipoulizwa Je ujenzi wa sasa unaendelea baada ya bei ya Saruji kushuka ? na wale ambao tayari wamekamilisha chini ya mradi huu, wao bei haikupanda ? Nakumbuka bei ilipanda Novemba,2020 sasa sababu hizi hazina mashiko katika hili" Amesema Remidius.
Afisa Tarafa ndani ya kikao hicho amelazimika kumpigia simu moja kwa moja Mweka hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino ambaye amefafanua na kuelezea "kufikia mwezi Agosti, 2020 mifumo wa fedha ilikuwa imefunguka tayari kwa matumizi sahihi ya fedha hizo" tofauti na madai ya Mwalimu mkuu huyo wa Shule amejaribu kujificha katika kivuli cha mfumo wa fedha.
Kijiji hiki mnayo bahati ya pekee, ni Kijiji cha Mwiyendaje ambacho Mhe.Rais Dkt John Pombe Magufuli Tarehe 26 Oktoba,2020 akiwa hapa Haneti amehadi kutatua changamoto ya Zahanati, Umeme, kuwajengea Daraja kubwa (Mwiyendaje - Kwahemu), Bwawa kwa ajili ya shughuli za kilimo na barabara hii ya Haneti - Zajilwa, sasa kama mnasusua katika miradi hii maana yake mnatia shaka kwa miradi mingine na kufanya kata na tarafa kutiliwa shaka" Remidius.
Katika hatua nyingine kiongozi huyo amewataka Mtendaji wa Kijiji na Kata pamoja na Afisa Elimu Kata hiyo na wao kueleza kwa maandishi kwa nini wameshindwa kusimamia kikamilifu mradi huo kupitia nafasi zao na kwamba walipaswa kufanya ufuatiliaji wa hatua zote za Mradi huo.
Mapema kabla ya kuwasili Mwiyendaje Afisa Tarafa amefanya ziara katika Shule ya Sekondari Haneti kwa lengo la kukagua na kupokea taarifa ya ujenzi na ukarabati wa vyumba vya madarasa pamoja na kufanya kikao cha ndani na kamati ya Ujenzi na kisha kupokea taarifa ya kuwasili kwa Wanafunzi shuleni hapo tangu kufunguliwa rasmi kwa shule zote nchini tarehe 11.01.2021.
Afisa Tarafa Itiso Remidius Emmanuel akizungumza na baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Shule na Serikali ya Kijiji cha Mwiyendaje baada ya kutofurahishwa na kusuasua kwa mradi wa EP4R (Ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa) vilivyokuwa vimetengewa Shilingi Milioni 40 ambazo tayari zilitolewa na Serikali na kuanza matumizi tangu Agosti, 2020.Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment