Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Daniel Chongolo akiwa ameambatana na Mstahiki Meya wa Wilaya hiyo Songoro Mnyonge wakikagua sehemu yanapojengwa majengo ya maduka katika makazi ya Magomeni kota, jijini Dar es Salaam.
Meneja wa mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi za Magomeni kota Benard Mayemba (kulia) akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Daniel Chongolo (wa pili kushoto) mara baada ya kufanya ziara ya ukaguzi wa mradi huo ambapo DC Chongolo ameipongeza TBA kwa ubunifu walioonesha katika ujenzi wa nyumba hizo, leo jijini Dar es Salaam.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Songoro Mnyonge (katikati) akitoa maelekezo kwa Meneja wa mradi huo Bernad Mayemba( kulia) wakati walipofanya ziara katika mradi wa nyumba hizo kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Daniel Chongolo, leo jijini Dar es Salaam.
Muonekano wa nyumba za makazi za Mgomeni kota ambazo zimekamilika kwa asilimia 90 na zitaanza kupokea wakazi mwishoni mwa mwezi huu jijini Dar es Salaam.
Ziara ikiendelea.
Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
MKUU wa Wilaya ya Kinondoni Daniel Chongolo amesema ubunifu wa kuweka huduma za kijamii walioonesha Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) katika nyumba za makazi Magomeni (Magomeni Kota,) umeiongezea thamani wakala hiyo na kwa kiasi kikubwa wakazi wa eneo hilo hawatapata changamoto za huduma za kijamii ikiwemo maji pamoja na maduka ya kupata mahitaji yao.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam mara baada kutembelea mradi huo ambao umekamilika kwa asilimia 90 na kubeba wakazi 644 Chongolo amesema;
"Ahadi aliyoihaidi Rais Magufuli inatekelezwa vyema, hatua iliyofikiwa ni nzuri na kaya zitarudi kuishi kwenye makazi yao, TBA mmetekeleza mradi huu kisasa zaidi na mmejiongeza kwa kujenga majengo ya huduma tumeona sehemu za maduka, sehemu za kupumzika na sehemu maalumu ya walinzi, mmeboresha vyema mradi huu." Amesema Chongolo.
Pia amesema, kutoka na usasa wa Majengo hayo Wakala hiyo lazima itoe elimu kwa wakazi watakaoingia kuishi humo juu ya matumizi ya vilivyomo pamoja na kuweka taratibu na hatua zitakazochukuliwa kwa watakaokiuka.
Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Meneja anayesimamia mradi huo Bernard Mayemba amesema, Wakala ya Majengo Tanzania (TBA,) imejipanga katika uwezeshaji na utekelezaji wa miradi mingi zaidi.
Pia amesema, mifumo awali ya umeme na maji umekamilika na hiyo ni pamoja na sehemu maalumu ya walinzi ambao watalinda makazi na wakazi wa eneo hilo kwa saa 24.
Mayemba amesema kuwa mradi huo umekuwa na manufaa kwa wakazi wa maeneo hayo ambapo kwa siku takribani vijana 700 hadi 800 wamekuwa wakipata ajira katika eneo hilo.
"Kuna vijana wengi ambapo wanapata kipato kupitia mradi huu, akina mama ntilie wapo hapa wakitafuta riziki....na katika kuokoa fedha za ndani viwanda vya kuchakata zege na tofali zipatazo Laki 9 zilizotumika kujenga mradi huu vilianzishwa na Wakala wa Majengo." Amesema.
Pia Mayemba amemshukuru Rais Magufuli kwa kuendelea kuiamini TBA na kuahidi kuendelea kufanya kazi kwa weledi zaidi.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment