DIWANI LUKA AMUOMBA WAZIRI JAFO KUUPANDISHA HADHI MJI MDOGO WA MIRERANI | Tarimo Blog

 

Diwani wa Kata ya Endiamtu, Mji mdogo wa Mirerani, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Lucas Chimbason Zacharia (kulia) akimkabidhi Mkuu wa shule ya sekondari Mirerani, Benjamin Mkapa, Samwel Kaitira moja Kati ya viti na meza 85 alizotengeneza kwa gharama ya shilingi milioni 2.9 ajili ya wanafunzi wa shule hiyo, katikati ni Ofisa mtendaji wa Kata ya Endiamtu, Charles Msangya na kushoto ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Tanesco, Justin Nyari.
Diwani wa Kata ya Endiamtu, Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Lucas Chimbason Zacharia (kushoto) akimkabidhi Mkuu wa shule ya sekondari Mirerani Benjamin Mkapa, Samwel Kaitira, moja kati ya viti na meza 85 alizotengeneza kwa gharama ya shilingi milioni 2.9 vitakavyotumiwa na wanafunzi wa shule hiyo, kulia ni Ofisa mtendaji wa Kata ya Endiamtu, Charles Msangya na Ofisa Tarafa ya Moipo, Joseph Mtataiko.

Diwani wa Kata ya Endiamtu Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Lucas Chimbason Zacharia akiwapongeza walimu na wanafunzi wa shule ya sekondari Mirerani Benjamin Mkapa kwa ufaulu mzuri wa matokeo ya kidato cha pili na cha nne.

Na Mwandishi wetu, Mirerani 

DIWANI wa Kata ya Endiamtu Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Lucas Chimbason Zacharia amemuomba Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI) Seleman Jafo aupandishe hadhi Mji mdogo wa Mirerani uwe Mji kamili au Halmashauri ya Wilaya ili kusogeza karibu zaidi huduma za jamii. 

Diwani mhe Luka Zacharia ameyasema hayo wakati akikabidhi viti na meza 85 za gharama ya shilingi milioni 2.9 kwa ajili ya wanafunzi wa shule ya sekondari Mirerani Benjamin Mkapa. Diwani huyo amesema endapo mji mdogo wa Mirerani ukipandishwa hadhi kuwa mji kamili au halmashauri, huduma za afya, elimu na sekta nyingine zitaboreshwa tofauti na ilivyo sasa. 
“Mirerani kuna idadi kubwa ya watu, kituo cha afya Mirerani kinapaswa kuwa hospitali kwani kwa siku moja kinahudumia watu 300 na kata ya Endiamtu shule za msingi zina wanafunzi 600, kata ziongezwe ili pawe mji kamili unaojitegemea,” amesema mhe Luka.Amesema hivi wananchi wa mji mdogo wa Mirerani hulazimika kusafiri umbali wa kilomita 120 hadi makao makuu ya wilaya hiyo Orkesumet ili kufuata huduma za kiwilaya.

Hata hivyo, mhe Luka amesema baada ya kusikia shule ya sekondari Mirerani Benjamin Mkapa ina changamoto ya viti na meza aliona atengeneze vipya na pia kukarabati vile vilivyoharibika.
“Nimezungumza na wadau wengine akiwemo Benki ya NMB Tawi la Mirerani ndugu yetu Kombe na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Yefred Myenzi ili tupate viti na meza nyingine,” amesema mhe Luka. 

Pia, amewapongeza walimu wa shule za msingi katika eneo hilo, kwani wamefaulisha wanafunzi wa darasa la saba wakashika nafasi tano za juu kwa kufaulisha na wanafunzi hao wameanza kidato cha kwanza mwaka huu. 

“Napenda kuwashukuru walimu wa shule ya sekondari Mirerani Benjamin Mkapa kwa kufaulisha division one wanafunzi tisa na division two wanafunzi 27 hongereni sana, sisi tutaonana na wazazi kuboresha shule na ninyi walimu mbaki kuhangaika na taaluma,” amesema Luka. 


Mkuu wa shule hiyo Samwel Kaitira akipokea viti na meza hizo amesema kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha nne na cha pili kinazidi kupanda baada ya matokeo kutangazwa juzi.
Kaitira alisema kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa juzi ya kidato cha nne, wanafunzi tisa walipata daraja la kwanza, 27 walipata daraja la pili, daraja la tatu 21, daraja la nne 63 na daraja sifuri ni 32.
“Kwa upande wa matokeo ya kidato cha pili wanafunzi 38 walipata daraja la kwanza, 29 daraja la pili, 47 la tatu, 58 la nne na wanafunzi wawili walipata daraja sifuri,” amesema Kaitira. 

Ofisa mtendaji wa kata ya Endiamtu, Charles Msangya amemshukuru Diwani huyo kwa kujitolea msaada huo wa viti na meza na kutoa wito kwa wadau wa maendeleo waige hilo. Msangya pia amewapongeza walimu wa shule hiyo kwa ufaulu mzuri wa matokeo ya kidato cha nne na cha pili yaliyotangazwa jana ila wasirudi nyuma waendelee kuwa imara zaidi. 

Ofisa Tarafa wa Moipo Joseph Mtataiko amewapongeza walimu wa shule hiyo na wanafunzi kutokana na matokeo mazuri ya ufaulu wa mitihani ya kidato cha nne na cha pili. “Ufaulu huu ni matokeo ya kambi mliyoweka kwa kuhakikisha wanafunzi wanasoma hadi usiku, wale wazazi waliokuwa wanapinga hilo watoto wao ndiyo wamefeli sasa,” amesema Mtataiko. 

Mmoja kati ya wanafunzi wa shule hiyo Cicilia Godlove amemshukuru diwani huyo kwa kuwapa viti na meza hizo ambazo zitawasaidia wakae kwenye mazingira mazuri wakati wa masomo yao.
“Tunakuahidi mheshimiwa Diwani kuwa tutavitunza viti na meza zake wakati wa masomo yetu na tutawasikikiza walimu vizuri ili tuelewe masomo na kufaulu,” amesema.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2