Mwandishi Wetu, Dodoma
MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mji wa Dodoma (DUWASA,) imefufua kisima cha maji kilichojengwa mwaka 1989 eneo la Nzuguni jijini Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Aron Joseph ametoa maelezo ya kisima hicho jana Jumapili tarehe 3 Januari 2020 mbele ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba aliyekuwa na ziara kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.
Joseph alisema, dhamira waliyonayo ni kuvifufua visima vya zamani ili visaidie kutoa huduma ambapo wameshavitambua visima 11 vilivyopo katikati ya Mji.
“Kisima hiki kilikuwepo tangu mwaka 1989 lakini kutokana na changamoto mbalimbali kilitelekezwa, dhamira yetu ni kuvitambua na kuvifufua visima hivi ili viweze kusaidia kutoa huduma ya maji kwa wananchi na hivyo kupunguza upungufu wa maji uliopo,” alisema Joseph.
Joseph alisema, matokeo ya majaribio ya kisima hicho, yameonyesha kitakuwa kina uwezo wa kutoa lita 8000 kwa saa na kwa siku lita 192,000.
Naye Mhandisi Nadhifa aliyetembelea miradi mbalimbali ikiwemo ya eneo la Ihumwa panapochimbwa visima, eneo la Nzughuni kunapofufuliwa kisima alisema ameridhishwa na utendaji kazi wa DUWASA.
“Hapa nimeridhishwa na menejimenti ya DUWASA, wamefanya jitihada kubwa ya kuhakikisha wananchi wanapata maji, kazi inayofanyika hapa ni kufufua visima ambavyo vilichimbwa zamani ni ubunifu mkubwa, hongereni sana,” alisema Mhandisi Nadhifa
Katika ziara hiyo, Mhandisi Nadhifa, alitoa siku 60 kwa mkandarasi SUMA JKT anayejenga tanki la maji eneo Buigiri wilayani Chamwino kuhakikisha anakamilisha kazi hiyo.
Tanki hilo la maji lenye ujazo wa wa lita milioni 2.5, linajengwa kwa gharama ya Sh.998 milioni na linatarajiwa kuhudumia wakazi wa Chamwino Ikulu, Hospitali ya Uhuru na Buigiri.
Mhandisi Nadhifa alisema, tanki hilo lilitakiwa lijengwe Septemba 2020 lakini limechelewa kukamilika.
“Tumekubaliana na mkandarasi kuwa tenki hili likamilike ndani ya miezi miwili (kuanzia jana), ili kuharakisha kazi hii, menejimenti ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (DUWASA) fuatilieni kazi hii kila siku ili mradi ukamilike kwa wakati,” aliagiza Mhandisi Nadhifa
Naibu katibu mkuu huyo, aliitaka DUWASA kuongeza kasi ya kukamilisha ufufuaji na uchimbaji wa visima hivyo ili wananchi wa Jiji hilo la Dodoma ambapo ni makao makuu ya nchi waondokane na usumbufu wa kukosa huduma hiyo muhimu.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment