Na Said Mwishehe, Michuzi TV
JESHI la Polisi limewaonya wamiliki wa magari ambao wamekuwa wakibadilisha vibao vya namba za magari(Plate Nomber) kwa ajili ya kukwepa kulipa madeni wanayodaiwa na Serikali baada ya kufanya makosa ya barabarani.
Onyo hilo limetolewa leo Januari 4,2021 na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini ,IGP Simon Sirro wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza kikao kati yake na askari Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani.
Kikao hicho kimefanyika katika Bwalo la Maofisa wa Polisi Oyestabay jijini Dar es Salaam ambako pamoja na mambo mengine walikuwa wakifanya tathimini za utendaji kazi wao katika mwaka 2020 na kuweka mikakati mipya kwa mwaka 2021.
Kuhusu wamiliki wa magari kubadilisha namba za magari ili kukwepa kulipa kodi, IGP Sirro amesema wamebaini kuna magari yamekuwa yakiwekwa yadi na wamiliki kwa lengo la kukwepa kulipa madeni ambayo magari hayo yanadaiwa kutokana na makosa yaliyofanywa na madereva barabarani.
" Kuna watu wanadaiwa lakini wanaficha magari nyumbani.Wengine wana gari zaidi ya moja, hivyo anachokifanya anabadilisha plate number na kusababisha kutosomeka katika mfumo wa kieletroniki.Wanafanya hivyo kukwepa kulipa madeni yanayotokana na makosa ya barabarani.
"Wenye tabia hii watambue Serikali ina mkono mrefu itawabaini na kuwachukulia hatua,nimeshatoa maelekezo ili tuweze kushughulika na hao wadanganyifu huu,"amesema IGP Sirro.
Akizungumzia ajali za barabarani, amesema kupitia tathimini waliyoifanya wamebaini wamefanikiwa kwa kiasi kukubwa kudhibiti ajali za barabarani kwa asilimia 34."Mwaka 2020 tumefanikiwa kupunguza ajali za barabarani, sote ni mashahidi trafiki wamefanya kazi nzuri.
"Hivyo tumeweka mkakati kwa mwaka 2021 tupunguze ajali za barabarani kwa asilimia 50, uhalifu wa barabarani kwa ujumla umepungua kwa asilimia 20."
Akizungumzia suala la maadili ndani ya kikosi hicho cha usalama barabarani, amesema bado kuna changamoto ya malalamiko ya rushwa na lugha mbaya kwa baadhi ya watumishi, hivyo wameweka mkakati kuhakikisha wanaondoa malalamiko ya uwepo wa rushwa.
Wakati huo huo amesema hakuna sababu ya trafiki kumuweka muda mrefu mtu ambaye amemkamata kwa makosa ya barabarani, ni vema mtu anapokamatwa basi asichukue muda mrefu labda liwe kosa ambalo limesababisha mtu kufa.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini ,IGP Simon Sirro akizungumza na Waandishi wa habari leo jijini Dar baada ya kumaliza kikao kati yake na askari Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani.
Baadhi ya Waandishi wa habari wakimsikiliza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini ,IGP Simon Sirro leo jijini Dar,baada ya kumaliza kikao kati yake na askari Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment