KUNAMBI ACHANGIA SH MILIONI TATU ZA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA UJENZI WA MADARASA, VISIMA VYA MAJI NA UMEME | Tarimo Blog


Charles James, Michuzi TV

KAZI inaendelea! Ndicho alichokisema Mbunge wa Jimbo la Mlimba mkoani Morogoro, Godwin Kunambi mbele ya wananchi wa Kata ya Kamwene na Mlimba ambazo zote amezitembelea na kutatua changamoto zao.

Mbunge Kunambi ambaye yupo kwenye ziara ya kikazi jimboni kwake amesema ziara yake hiyo siyo tu ya kuwashukuru wananchi kwa kumchagua yeye na Rais Dk John Magufuli na madiwani bali pia ni kutatua changamoto zinazowakabili wananchi hao.

Katika kata ya Kamwene, Kunambi ametembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa kwa nguvu za wananchi na kuichangia lakini pia akizindua kisima cha Maji katika Shule ya Msingi Kamwene.

Kunambi amechangia kiasi cha Sh Milioni Tatu katika Kata ya Kamwene jimboni kwake ambazo zitaelekezwa kwenye miradi ya ujenzi wa madarasa katika Sekondari ya Kamwene, kutatua changamoto ya Umeme katika Kijiji cha Viwanjasita pamoja na mifuko ya saruji kusaidia ujenzi wa miradi ya maji jimboni humo.

" Hii ni siku ya pili ya ziara yangu nimetembelea kata ya Kamwene na kukutana na changamoto ya ujenzi wa madarasa, mimi kama Mbunge wenu nachangia kiasi cha Sh Milioni Moja niwapongeze kwa jitihada mlizofanya, hii Zahanati ya Viwanjasitini nayo ina changamoto ya Umeme napo nimetoa Sh Milioni Moja ili umeme uletwe hapa Mama zetu na Baba zetu watibiwe hapa.


" Wenyeviti wangu wa vijiji viwili vya kata hii mliomba mifuko 15 kila mmoja ya saruji kukamilisha ujenzi wa visima vya maji leo hii hii fedha za mifuko hiyo nawapa na ujenzi uendelee wananchi wetu wanywe maji, licha ya kutoa 1m ya umeme kwenye zahanati pia kuna shida ya maji nitaenda kukaa na wenye mamlaka na ndani ya muda mfupi mtaona matokeo," Amesema Mbunge Kunambi.

Akiwa katika Kata ya Mlimba mbunge huyo amepokea changamoto ya Maji ambapo wananchi wa kata hiyo walimueleza ili Changamoto hiyo imalizwe ni vema waletewe Pampu kubea inayosukuma maji jambo ambalo Meneja wa Ruhasa alilifanyia kazi hapo hapo kwa pampu hiyo kwenda kuchukuliwa na kuletwa ili ifungwe.

" Mlimba tulichelewa sana niwahakikishie kazi ndio imeanza, kuna sehemu nimebip tu nimeletewa mradi wa usanifu wa michoro na upembuzi yakinifu wa mradi wa barabara wa kiwango cha lami km 223 huu ni mradi wa kujua gharama za ujenzi wa hiyo barabara na tenda ishaanza baada ya kukamilisha kazi hii sasa tutaomba fedha za utekelezaji na naamini tutapata," Amesema Kunambi.

Kwa upande wao wananchi wa kata hizo mbili wamemshukuru Mbunge wao kwa jitihada zake hizo licha ya kuwa na miezi miwili tu tangu aapishwe huku wakimhakikishia kumpa ushirikiano na kumuombea katika utekelezaji wa majukumu yake ya kibunge.

Mbunge wa Jimbo la Mlimba mkoani Morogoro, Godwin Kunambi akikagua miundombinu ya barabara zilizopo katika kata ya Mlimba ambapo kwa kushirikiana na TARURA wameahidi kuanza kuzifanyia kazi ili zisiwe kikwazo cha wanafunzi kwenda shule nyakati hizi za mvua.
Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Godwin Kunambi akizindua kisima cha maji katika Shule ya Msingi Kamwene kata ya Kamwene ambapo pia amechangia Mifuko 30 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa visima vingine viwili vya kata hiyo.
Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Godwin Kunambi akizungumza na wananchi wa Kata yake ya Kamwene akiwa ziarani kwenye kata hiyo kutatua changamoto mbalimbali.
Wananchi wa Kijiji cha Viwanjasita wakimsikiliza Mbunge wao Godwin Kunambi ambaye amefika kutatua changamoto zao huku akichangia Sh Milioni Moja ili kuweza kuvutwa umeme kwenye Zahanati ya Kijiji hiko.
Mbunge wa Mlimba Godwin Kunambi akiangalia ujenzi wa maboma ya madarasa ya Shule ya Sekondari Kamwene uliokwama ambapo ametoa kiasi cha Sh Milioni Moja kumalizia ujenzi huo.
 
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2