MAABARA YA TMDA KANDA YA ZIWA KUWA MAABARA BOBEZI KWA VIPUKUSI | Tarimo Blog


Kaimu Meneja Kanda ya Ziwa wa Mamlaka ya  Dawa na Vifaa Tíba (TMDA) Sophia Mziray akizungumza na waandishi Habari kuhusiana na Maabara bobezi katika Vipukusi wakati waandishi walipotembelea Maabara hiyo jijini Mwanza.
Kaimu Mkuu wa Maabara wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Bugusu Nyamweru akitoa maelezo kuhusiana mtambo wa kutenganisha kiwango cha Pombe katika kipukusi (Steam Distller) wakati uchunguzi wa Vipukusi katika Maabara hiyo jijini Mwanza.
Mtaalam wa Maabara wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA,) Kanda ya Ziwa Jovenas Rwezaura akitoa maelezo wakati wa uchunguzi wa Pombe katika Kipukusi .


*Kaimu Meneja ataja vigezo vya kufikia ubobezi katika Maabara

Na Chalila Kibuda, Michuzi TV- Mwanza 

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imeiteua Maabara yake ya Kanda ya Ziwa kuwa Maabara Bobezi katika chunguzi za Vipukusi. 

Uwepo wa  Maabara bobezi kwa Vipukusi itakuwa na faida kwa nchi na kufanya baadhi nchi zingine kutumia Maabara hiyo kwa kulipa tozo mbalimbali katika mamlaka.

Akizungumza na waandishi wa Habari waliotembelea Maabara hiyo Kaimu Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa Sophia Mziray amesema hatua zilizopo ni kuwajengea uwezo wataalam na kuimarisha baadhi ya miundombinu pamoja na kukamilisha hatua mbalimbali za kaguzi kwa wanaotoa idhibati ya maabara bobezi kwa viwango vilivyowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO.)

Mziray amesema kuwa,  Maabara hiyo ikiwa bobezi itafanya baadhi ya nchi kutumia katika kufanya chunguzi za Vipukusi vyao kwa kulinda wananchi wao kwa kuwa na Vipukusi vyenye usalama, ubora pamoja na ufanisi.

Aidha, amesema  kufikia ndani ya miaka mitatu ya awamu ya Pili ya Rais Dkt.John Pombe Magufuli moja ya hatua kubwa kwa Mamlaka ni  kuwa na  Maabara bobezi  ambayo itahudumia Tanzania na baadhi ya nchi jirani na za Kikanda kama SADC na EAC. 

"Tumejipanga kuwa na Maabara bobezi kwa ajili ya Vipukusi kutokana na kuwa na mahitaji makubwa katika Sekta ya Afya katika suala la zima la utakasaji wa mikono na Vifaa Tiba katika utoaji huduma za afya." Amesema Mziray.

Hata hivyo Kaimu Meneja amesema kuwa na Maabara bobezi ni faida ya nchi kwani baadhi ya Vipukusi vitatengenezwa ndani ya nchi na kupeleka nje na kubaki kuwa fahari ya nchi na sio TMDA pekee ambao kazi yetu ni kuhakikisha wanalinda  afya ya jamii kupitia udhibiti wa ubora, usalama na ufanisi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2