OLE LEKAITA ATEMBEA KILOMITA TANO NA KUPANDA MLIMA WA MITA 2,200 KUKAGUA CHANZO CHA MAJI | Tarimo Blog

 

Mbunge wa Jimbo la Kiteto, Mkoani Manyara, Edward Ole Lekaita (wapili kushoto) akipanda mlima umbali wa mita 2,200 usawa wa bahari ili kukagua chanzo cha maji kwenye Kata ya Dongo.
Mbunge wa Jimbo la Kiteto Mkoani Manyara, Edward Ole Lekaita (katikati aliyevaa kofia) akikagua eneo la chanzo cha maji kwenye Kata ya Dongo.
 
………………………………………………………………………………….
Na Mwandishi wetu, Kiteto
MBUNGE wa Jimbo la Kiteto Mkoani Manyara, Edward Ole Lekaita amelazimika kupanda mlima wenye urefu wa mita 2,200 kwa kutembelea kwa miguu umbali wa kilomita tano ili kukagua chanzo cha maji kwenye Kata ya Dongo ambapo wananchi wana changamoto ya maji.
Ole Lekaita ametembelea eneo hilo akiwa kwenye ziara yake ya kutembelea wananchi na kubaini changamoto na kuona mafanikio chanya ya wapiga kura wa jimbo lake.
Amesema alilazimika kupanda kutembelea eneo hilo la chanzo cha maji ambapo kutajengwa bwawa kubwa la maji litakalohudumia binadamu na mifugo wa kata za Dongo na Laiseri.
Amesema kero ya maji imekuwa sugu kwa wananchi wa eneo hilo hivyo amefika ili aweze kuona namna ya wananchi wataondokana changamoto hiyo.
“Mradi wa bwawa hili kubwa utakapokamilika utasaidia wananchi wa kata za Dongo na Laiseri ambazo zipo pembezoni na zina uhitaji makubwa wa maji,” amesema Ole Lekaita.
Amesema amewasiliana kwa njia ya simu na meneja wa mamlaka ya maji vijijini (Ruwasa) wa wilaya ya Kiteto ambaye amemuhakikishia ndani ya wiki moja atatembelea mradi huo.
“Nitakutana na meneja wa Ruwasa ili tuweze kuboresha mradi na wananchi watatuliwe kero ya maji ambayo imekuwa sugu kwa wananchi wa kata ya Dongo,” amesema Ole Lekaita.
Hata hivyo, mkazi wa kijiji cha Dongo, Juma Mwadimange amempongeza mbunge huyo kwa jitihada zake za kufuatilia kero za wananchi hadi kupanda mlima na kufika kwenye chanzo cha maji.
“Wananchi wa jimbo la Kiteto hawakufanya makosa kumchagua Ole Lekaita kuwatumikia kwani ameonyesha imani kubwa hadi kupanda mlima na kutembelea umbali mrefu na kufika kwenye chanzo cha maji,” amesema Mwadimange.
Akiwa kwenye ziara ya kata ya Dongo, mbunge huyo pia ametembelea shule ya msingi Dongo, shule ya msingi Chang’ombe na zahanati ya Dongo na kuzungumza na wananchi wa eneo hilo.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2