WAKUU WA IDARA ZA SERIKALI WATAKIWA KUJUA MIPAKA YAO YA KAZI NA KUZIJUA SHERIA LUDEWA MKOANI NJOMBE | Tarimo Blog

 Na Shukrani Kawogo, Njombe.

Wakuu wa idara mbalimbali za serikali  wilayani  Ludewa mkoani Njombe wametakiwa kujua mipaka yao ya kazi  na kuzijua sheria zinazowalinda ili waweze kufanya kazi kwa kujiamini na kwa ufanisi zaidi.

Hayo ameyasema mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga alipokuwa kwenye mkutano na wakuu wa idara hizo uliohudhuliwa na viongozi mbalimbali wa ngazi ya wilaya.

Amesema endapo wakuu hao wakizijua vyema sheria zinazowalinda itawasaidia kufanya kazi kwa kujiamini pasipo kupelekeshwa na mtu wala kuingilia majukumu yao.

Ameongeza kuwa shughuli zake zinauhusiano mkubwa sana na wakuu wa idara mbalimbali hivyo ameomba kuonyesha ushirikiano wao kwake na madiwani ili waweze kuleta maendeleo Ludewa.

"Kila mkuu wa idara anapaswa kuwa mstari wa mbele katika kufanya jambo litakaloiletea Ludewa Maendeleo, hampaswi kuwa waoga katika kufanya maamuzi ni vyema ukaamua kutekeleza jambo na utakapokosea utarekebishwa kuliko kutotekeleza kabisa", alisema Kamonga.

Aidha kwa upande wa mkuu wa wilaya hiyo Andrea Tsere amesema kila idara inapaswa kubuni mbinu mbalimbali zitakazo wawezesha kuongeza ubora na ufanisi katika kazi.

Amesema wilaya inapofanya vizuri katika nyanja mbalimbali ni pongezi kwa kila idara iliyohusika katika kusukuma Maendeleo hayo hivyo ni vyema washirikiane ili waweze kuleta mabadiliko.

Aliongeza kuwa wahandisi wa idara mbalimbali pia wanapaswa kushirikiana na kupeana ushauri katika miradi mbalimbali ya ujenzi inayoendelea kwani kwa kufanya hivyo kutapelekea kuwa na ujenzi wenye kiwango kizuri.
 
Naye katibu ya chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo, Bakari Mfaume amewataka wakuu hao kutekeleza majukumu yao kwa kufuata ilani ya chama hicho ili kuendana na misingi ya utekelezaji ulioanisha katika ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

Amesema ilani hiyo ndiyo inayolinda mwenendo wa serikali na ndiomaana Rais John Pombe Magufuli ameunda serikali inayoendana na ilani ya chama hicho.

"Rais alipounda wizara ya sayansi teknolojia na ubunifu wengi walisema ameunda wizara mpya lakini katika sura ya nne ya ilani hiyo inahusu teknolojia ya sayansi na ubunifu na katika ibara ya 101 imeeleza juu ya utekelezaji wa ilani hiyo", alisema Mfaume.

Ameongeza kuwa hivyo wakuu wa idara wanapaswa kujua makubaliano ya chama na wananchi ili katika utendaji wao watende kwa kufuata makubaliano hayo ambayo yanatoka ndani ya ilani ili kuleta maendeleo kwa jamii.

Mkuu wa wilaya ya Ludewa, Andrea Tsere akiongea na wakuu wa idara mbalimbali za serikali wa wilaya hiyo (hawapo pichani) katika mkutano uliofanywa kati ya wakuu hao na viongozi wa serikali.

Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga, akiongea na wakuu wa slekta mbalimbali za serikali wa wilaya ya Ludewa (hawako pichani)
Wakuu wa idara mbalimbali za serikali wilayani Ludewa wakimsikiliza mkuu wa wilaya hiyo Andrea Tsere katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri wilayani humo.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa Sunday Deogratius (kulia) akiongea na wakuu wa idara mbalimbali wilayani humo(hawapo pichani). Anayefuata ni mwenyekiti wa halmashauri Wise Mgina, mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga pamoja na mkuu wa wilaya hiyo Andrea Tsere.
Katika wa CCM wilaya ya Ludewa Bakari Mfaume akiongea na wakuu wa idara mbalimbali wa wilaya hiyo(hawapo pichani) kushoto kwake ni mwenyekiti wa CCM wilaya hiyo Stanley Kolimba, kamanda wa polisi wilayani humo Deogratius Masawe pamoja na mkuu wa wilaya hiyo Andrea Tsere.
Wakuu wa idara mbalimbali za serikali wilayani Ludewa wakifiatilia mijadala mbalimbali iliyokuwa ikitolewa na viongozi wa serikali katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa halmashauri wilayani humo.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2