WAZIRI MALIASILI NA UTALII AFANYA ZIARA SHAMBA LA MITI BIHARAMURO- CHATO, AWAPONGEZA TFS KWA KAZI WANAYOFANYA | Tarimo Blog

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Damas Ndumbaro (mwenye miwani) akimsisitiza Kamishna wa Uhifadhi TFS Prof. Dos Santos Silayo (mwenye kombati) kufanya uwekezaji wa miundombinu ya utalii katika Shamba la Miti Biharamulo Chato ili kuweza kujiingizia kipato kwa shughuli za utalii alipofanya ziara ya kikazi katika Shamba la Miti Biharamulo Chato Januari 12,2021. Wa kwanza kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Aloyce K. Nzuki na wengine ni watendaji wa TFS.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Damas Ndumbaro (mwenye miwani) akijadiliana jambo na Kamishna wa Uhifadhi TFS Prof. Dos Santos Silayo (mwenye kombati) wakati wa ziara katika Shamba la Miti Biharamulo Chato iliyofanywa na Waziri huyo akiwa na watendaji wengine .

WAZIRI wa Maliasili na Utalii Dk.Damas Ndumbaro leo Januari 12 , 2021 amefanya ziara katika Shamba la Miti Biharamulo – Chato Geita ikiwa ni ziara ya kawaida ya kazi iliyolenga kujitambulisha na kukagua utendaji kazi wa Taasisi hiyo.

Katika ziara hiyo Dk. Ndumbaro aliyembatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Aloyce Nzuki ameupongeza  Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) kwa kazi kubwa ya upandaji miti iliyoifanya katika Shamba la Miti Biharamulo Chato lakini pia katika maeneo mbalimbali ya nchi.

“Niwapongeze sana TFS kwa kazi kubwa mlioifanya na mnayoendelea kuifanya tangu kuanzishwa kwenu, leo nimeona shamba kubwa la miti iliyopandwa na kustawi vizuri bila kuharibiwa kwa watani wangu Wasukuma hii si kawaida, niwaombe watani zangu tulitunze shamba hili,

“Nimeelezwa kuwa ni shamba la pili kwa ukubwa nchini baada ya lile la Sao Hill Mafinga mkoani Iringa, hakuna asiyejua jinsi wakazi wa Mafinga wanavyonufaika na uwepo wa shamba la Sao Hill na sisi tunahadi uwanja wa ndege hapa tufungue fursa za utalii hapa, nimeshamuagiza Kamishna wa Uhifadhi TFS ajenge ‘Hostel’ na kutenga maeneo kwa ajili ya camping kwa watalii na wale wote wanaohitaji kujifunza kilimo cha miti biashara,” anasema Dk. Ndumbaro.

 Kwa upande wake  Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Biharamulo Chato, Geita Thadeus Shirima anasema hadi sasa jumla ya hekta 2682 sawa ekari 6705 zimeshapandwa miti ya kibiashara ambapo takribani watu 800 kila mwaka hupata ajira za muda kwa ajili yakutekeleza shughuli mbalimbali za shamba.

“Tangu kuanza shughuli za upandaji miti mwaka 2017/2018 tumekuwa tunatoa ajira za muda kwa wananchi wa vijiji vinavyozunguka, tunaruhusu wananchi kulima mazao ya chakula katika maeneo ya ambayo tayari yamepandwa miti na ambayo yanatategemea kupandwa ili kuboresha mahusiano na wananchi,” anasema Mhifadhi Shirima.

Aidha Kamishna wa Uhifadhi kutoka TFS Prof. Dos Santos Silayo anasema uanzishwaji na uendelezaji wa shamba hilo unaenda sambamba na malengo ya serikali ya awamu ya tano ya kuwa na uchumi wa viwanda kwani malighafi itakayopatikana katika shamba hilo itatumika katika viwanda vya misitu vyenye uwezo wa kuajiri watu wengi na uwezo wa kuzalisha bidhaa zinazotumiwa ndani ya nchi na ziada kuuzwa nchi za nje.

“Mhe. Waziri shamba hili linakwenda kuleta mapinduzi makubwa ya uchumi hapa Chato lakini kwa nchi kwa ujumla kutokana na kuotesha na kuuza miti ya mbao laini na ngumu kwa ajili ya kutoa malighafi kwa viwanda vya misitu lakini kwa maelekezo uliyotoa tunakwenda sasa kutekeleza ili tuweze kuuza mazao ya misitu na huduma mbalimbali huku tukiendelea kutoa ajira kwa wananchi,” anasema Kamiashna Prof. Silayo.
 
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2