BENKI KUU YA TANZANIA (BoT) YATOA TAARIFA KUHUSU MFUMO WA KIELETRONIKI WA USAJILI WA VIKUNDI VYA KIJAMII VYA HUDUMA NDOGO ZA FEDHA | Tarimo Blog

Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuufahamisha Umma kuwa imeandaa mfumo wa kieletroniki wa usajili wa vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Mfumo huu wa kielektroniki unalenga kuviwezesha vikundi vyote vya kijamii vya huduma ndogo za fedha kuwasilisha maombi ya usajili kwa njia ya kielektroniki, na unapatikana kupitia https://cmg.bot.go.tz/cmg-portal/login.

Mwongozo wa kuwasilisha maombi ya usajili wa vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha kupitia mfumo wa kieletroniki pamoja na fomu zinazohusu maombi ya usajili  vimewekwa kwenye kurasa za mfumo huu kwa ajili ya rejea kwa watumiaji.

Hivyo basi, vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha vinashauriwa kuanza kuwasilisha maombi ya usajili katika halmashauri husika ili yaweze kufanyiwa kazi na Mamlaka za Serikali za Mitaa kabla ya tarehe 30 Aprili 2021, ambayo ndio siku ya mwisho (kwa mujibu wa Sheria) ya kupokea maombi ya usajili kwa vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za kifedha vilivyokua vikifanya shughuli zake. Aidha, pale ambapo kikundi cha kijamii cha huduma ndogo za fedha kitapata changamoto kufanya usajili kwa njia ya kielektroniki, inashauriwa kipeleke maombi hayo kwa Afisa Maendeleo ya Jamii aliyeko katika Ofisi ya Kata au Halmashauri iliyo karibu kwa ajili ya msaada zaidi.

Benki Kuu kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa inapenda kuvitaarifu vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha kuhakikisha kuwa vinawasilisha maombi ya usajili kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa husika kabla ya tarehe 30 Aprili 2021. Aidha, kikundi chochote kitakachoendelea kufanya biashara ya huduma ndogo za fedha bila kuwa kimewasilisha maombi ya usajili, kitakuwa kinavunja Sheria na hivyo kitachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa Sheria. 

Usajili wa vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha ni utekelezaji wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya 2018 inayolenga kuhakikisha kuwa sekta ya huduma ndogo za fedha inasimamiwa vizuri ili iweze kuwa imara na kuchangia juhudi za Serikali za kuongeza upatikanaji wa huduma za fedha na kupunguza kiwango cha umasikini katika jamii ya Watanzania.

Benki Kuu ya Tanzania kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa iko tayari kutoa msaada utakaohitajiwa na kikundi chochote cha kijamii cha huduma ndogo za fedha kupitia nyamkoro.tanda@tamisemi.go.tz; bmnkwabi@bot.go.tz; zahara.msangi@tamisemi@go.tz;  dasasya@bot.go.tzna vctarimu@bot.go.tz


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2