DKT.NDUGULILE ATOA MAELEKEZO YA KUBORESHA MIFUMO YA TEHAMA NCHINI | Tarimo Blog



Na Faraja Mpina, WMTH, Dodoma

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile ametoa maelekezo kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula kuitisha kikao cha wataalamu wa mifumo ya TEHAMA siku ya tarehe 31/03/2021 kitakachoongozwa na wataalamu kutoka katika Wizara hiyo kwa lengo la kufanya tathmini ya mifumo ya TEHAMA ya kifedha iliyopo nchini.

Akizungumza katika kikao chake na waandishi wa habari katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma, Dkt. Ndugulile amesema kuwa amechukua hatua hiyo kutokana na Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na ripoti ya Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Fedha za Serikali (CAG), Dkt. Charles Kichere iliyowasilishwa kwake kuonesha kuna changamoto katika mifumo hiyo na Wizara yake imechukua jambo hilo kwa uzito mkubwa.

“Nimemuelekeza Katibu Mkuu wangu kuchukua hatua za haraka kwa kuitisha kikao cha wataalamu wa TEHAMA ili kufanya tathmini ya mifumo hiyo, idadi yake, changamoto za utengenezaji, uendeshaji na uendelezaji wa mifumo hiyo hapa nchini pamoja na changamoto ya mifumo hiyo kutosomana na kutobadilishana taarifa”, alieleza Dkt. Ndugulile

Aidha, alisisitiza kikao hicho kuwahusisha wataalamu kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora; Ofisi ya Rais - TAMISEMI; Wizara ya Fedha na Mipango; Ofisi ya Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Fedha za Serikali; Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA); Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL); Kituo cha Kuhifadhi Data cha Taifa (NIDC); Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).

“Natoa wiki moja kwa wataalamu hawa kufanyia kazi jambo kubwa lililogusiwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan la changamoto ya mifumo hiyo kuruhusu mianya ya upotevu wa mapato na usalama wa mifumo hii na kutoa mapendekezo ya maboresho ya nini kifanyike ili kuhakikisha mianya hiyo inazibwa, usalama wa mitandao unakuwepo na kunakuwa na mifumo inayosomana ambayo haitaruhusu kupoteza mapato ya nchi”, alisisitiza Dkt. Ndugulile

Aliongeza kuwa Wizara yake itafanyia kazi mapendekezo hayo ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za kuboresha na yale ambayo yatahitajika kushughulikiwa na mamlaka ya juu yatachukuliwa na kupelekwa kwa hatua nyingine zaidi.

“Jukumu kubwa la Wizara hii ni kutoa miongozo, usimamizi wa mifumo , uendelezaji na kuhakikisha nchi inakuwa na matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA na usalama wake, mifumo mingi iliyokuwa inatumiwa na Serikali ilikuwa inatoka nje ya nchi na fedha nyingi zilitumika kwa uendeshaji na kulipia leseni lakini kwa sasa zaidi ya asilimia 80 ya mifumo inayotumika nchini na ndani ya Serikali imetengenezwa na wataalamu wetu wazalendo”, alisisitiza Dkt. Ndugulile

Alisema kuwa jukumu kubwa alilonalo katika Wizara hiyo ni kuhakikisha inajenga uwezo wa wataalamu wa ndani ya nchi kuhakikisha mifumo mingi inaweza kutengenezwa hapa hapa nchini katika ubora unaoendana na mahitaji ya nchi na usalama dhidi ya udukuzi ambao unaweza kufanyika kwa kutumia mifumo ya iliyotengenezwa mahali pengine.

“Naomba niwaambieni kuwa TEHAMA ni sehemu ya siasa, biashara, ni masuala ya kiusalama na sisi kama Wizara tuna jukumu la kuhakikisha sekta za kiuchumi na fedha zinakuwa na mifumo imara, sekta za huduma ya kijamii kama vile afya, elimu na maji zinakuwa na mifumo salama na sekta zinazohusika na mambo ya ulinzi na usalama nazo zinakuwa na mifumo salama ili hata pale panapokuwa na changamoto kuhakikisha huduma za nchi zinaendelea pasipo kuathirika”, alimalizia Dkt. Ndugulile.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Bunge Jijini Dodoma. Kushoto ni Mulembwa Munaku, Mkurugenzi wa TEHAMA wa Wizara hiyo na kulia ni Prosper Minja, Afisa Habari wa Bunge.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Bunge Jijini Dodoma.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Bunge Jijini Dodoma. Kulia ni Prosper Minja Afisa Habari wa Bunge

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2