JAJI MSTAAFU DK. BWANA AMLILIA DKT. MAGUFULI | Tarimo Blog

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji Mstaafu, Mhe. Dk. Steven James Bwana (pichani) amesikitishwa sana na kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli na amesema kuwa Watanzania tumepata pigo kubwa kwa Serikali, Taifa na Afrika kwa ujumla. Tumempoteza Kiongozi bora, mahiri, shupavu ambae hakusita kuchukua maamuzi kwa maslahi ya taifa.

Dk. Bwana amesema hayo Jijini Dar es Salaam leo wakati wa mahojiano maalum huku akionesha kuhuzunishwa sana na msiba huu.  Alisema, “Hayati Rais Magufuli atakumbukwa daima. Katika kipindi cha uhai na uongozi wake amefanya kazi kubwa sana, wenye macho wanaona, ni mengi aliyoifanyia Nchi hii. Ameacha alama na kumbukumbu kubwa kwa Watanzania, katika nyanja mbalimbali. Alikuwa ni Kiongozi bora aliyejitoa kuwatumikia wananchi wake kwa umahiri, bidii na uzalendo kwa lengo la kuwaletea maendeleo wananchi, Taifa na katika kuendeleza uchumi wetu” alisema.

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Mheshimiwa Dk. Bwana amesema binafsi atamkumbuka kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kurejesha imani ya wananchi kwa Serikali yao kwa kusimamia haki. Alirejesha na kuongeza nidhamu na utendaji wa kazi, uwajibikaji na utawala bora katika utumishi wa umma, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha watumishi wa umma wanatoa huduma bora kwa wananchi.

Dkt. Bwana amesema Hayati Magufuli alifanikiwa pia kuboresha miundo mbinu ya huduma za afya, elimu, na barabara ili kuiunganisha Nchi na kurahisisha usafiri, yote yanaonekana.

Mheshimiwa Jaji Mstaafu Dk. Bwana amesema kwake binafsi atamkumbuka Hayati Rais Magufuli, mosi kama Rais ambae alikuwa mpole, mnyenyekevu, asiye kuwa na makuu. Pamoja na kuwa Kiongozi alikuwa mtu wa kawaida na kila mara walipokutana kwa nyakati tofauti alikuwa ni mtu wa kawaida. Alikuwa tayari kusikiliza shida na matatizo ya watu wote na kuwasaidia.

Akielezea zaidi alisema “Nakumbuka wakati alipoteuliwa kwa mara ya kwanza kugombea nafasi ya Urais kupitia Chama chake mwaka 2015, nilikuwa natoka nje ya Nchi, Cambodia. Nikiwa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, kupitia kwa Msaidizi wangu, nilipata taarifa ya kuteuliwa kwa Mheshimiwa Magufuli. Binafsi nilifurahi sana, furaha yangu ilitokana na mimi kumuona kuwa alikuwa ni mtu ambae alikuwa ni chaguo sahihi  na nilikuwa na imani nae sana”.

Pili, nitamkumbuka Rais Magufuli kwa sababu alionyesha imani kubwa sana kwangu mimi binafsi. Aliniona kuwa ni miongoni mwa watu ambao wangeweza kumsaidia, na akaamua kuniteua kwa mara ya pili mwezi Novemba 2018 kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma.

Dk. Bwana alihitimisha kwa kusema kuwa ana imani kubwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na Viongozi  wengine kuwa watasimamia kikamilifu aliyoyaanzisha na wataendelea kuchapa kazi kwa bidii na umahiri kuanzia pale alipoishia.

“Tuendelee kuomboleza kifo cha mpendwa wetu Hayati Dk. John Pombe Joseph Magufuli kwa kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ailaze Roho yake mahali pema peponi” alisema.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2