KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI YATOA KONGELE KWA WIZARA YA MADINI | Tarimo Blog

Na Tito Mselem, Mirerani
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imefurahishwa na juhudi za maendeleo zinazotekelezwa na Wizara ya Madini ambapo wameridhishwa na miradi inayoendelea kufanyika ndani ya Ukuta unaozunguka migodi ya Tanzanite Mirerani.

Kamati hiyo, imefanya ziara ndani ya Ukuta unaozunguka migodi ya Tanzanite Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara yenye lengo la kukagua miradi ya Tanzanite inayoendelea ndani ya ukuta huo.

Akizungumza kwenye ziara hiyo Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dustan Kitandula amesema, miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa ukiwemo mradi wa utengenezaji barabara ndani ya ukuta, kamera na taa zinazozunguka ukuta huo.

“Tunampongeza Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwajengea ukuta huu ambao kwa sasa tunaona mafanikio yake utoroshaji umepungua na thamani ya Tanzanite imeongezeka,” alisema Kitandula.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini Doto Biteko ameipongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa kufanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya Mirerani.
Akijibu swali la Mjumbe wa Kamati hiyo Joseph Musukuma, Waziri Biteko amesema, wito wa uongezaji thamani madini hapa nchini umezidi kuongezeka ambapo amesema mwaka 2017 kulikuwa na mashine za kukatia madini ya Tanzanite zisizozidi 120, mwaka 2021 kuna zaidi ya mashine 380.

“Rais wa Nchi hii anataka kuona watanzania wananufaika na madini waliyojaliwa na Mwenyezi Mungu, anataka kuona mabilionea wanatoka hapa hapa nchini,” aliongeza Waziri Biteko.

Naye, Mjumbe wa Kamati hiyo Jesca Mambatavangu amesema, baada ya Wizara ya Madini kulieleza Bunge la Jamhuri wa Tanzania utekelezaji wa miradi mbalimbali sasa Kamati inaitembelea ili ijiridhishe na utekelezwaji wake.

“Kwa kweli tumeiona miradi yote iliyokuwa inazungumzwa Bungeni na tumeridhika na utekelezwaji wake, tumeona wachimbaji wadogo wanatumia vifaa vya kisasa kwa kweli ni maendeleo makubwa,” alisema Mambatavangu.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2