Baadhi ya wanafunzi waliofanikiwa kufanya mtihani wao wa kutainiwa mafunzo ya udereva wa magari ya abiria katika chuo cha udereva mpechi wakiendelea na zoezi la upigaji wa picha kwa ajili ya kutumika kwenye vyeti vyao.
Na Amiri Kilagalila,Njombe
MADEREVA wa jinsia ya kike wanatajwa kuwa na uwezo mkubwa wa kuchukua tahadhari na kuepuka ajali za barabarani ukilinganisha na wanaume kutona na ajali ambazo zimekuwa zikitokea mara kwa mara huku sababu mbali mbali ikiwemo kujiamini kupita kiasi,ulevi na uzembe vikitajwa chanzo cha ajali za barabarani zinazosababishwa na wanaume.
Mkufunzi kutoka chuo cha Taifa cha usafirishaji mwalimu Frolian Alexanda Sonya amebainisha hayo mara baada ya kukamilisha usimamizi wa mitihani kwa madereva zaidi ya 20 wa magari waliokuwa wakipata mafunzo katika chuo cha udereva mpechi kilichopo Uwanja wa sabasaba mjini Njombe ambacho kinatoa elimu kwa wamiliki na wasafirishaji wa vyombo vya moto.
“Dereva wa kike umakini wao barabarani upo juu sana lakini walio wengi hawajiamini na laiti tungeweza kutoa mafunzo kwa jinsia hii kwa kiasi kikubwa pengine hizi ajali barabarani ingekuwa ni za kuskia tu,na mpaka sasa si chini ya wanawake 400 tumeshaweza kuwajengea uwezo kwasababu umakini wao ni wajuu sana ukilinganisha na wanaume”alisema Frolian Alexanda Sonya
Aidha amewataka madereva wakiwemo wa abiria kuendelea kupata elimu ya kujitambua na kujiheshimu pamoja na kubadilika kitabia ili kuepuka kufanya kazi kwa mazoea na wakati mwingine kuepuka kusababisha ajali zinazoweza kuepukika
Mkurugenzi wa chuo cha udereva Mpechi mjini Njombe Bi. Abiya Mpangile amesema chuo hicho kinaendelea kutoa fursa kwa kila dereva kupatiwa elimu kabla ya kuendesha vyombo vya moto pamoja na kutoa mchango katika kutokomeza matukio ya ajali za barabarani na kutoa wito kwa wamiliki wa magari kuajili madereva waliokwisha kusoma.
Aidha kuhusu wanafunzi wa jinsia ya kike amesema chuo hicho kimekuwa kikipokea wanafunzi wa jinsia mbali mbali wakiwemo wa jinsia hiyo huku akipongeza umakini wao wanapokuwa bara barani.
“Wakina barabarani huwa tunakuwa makini sana tofauti na hawa wenzetu kwa kuwa kujiamini kwao kunakuwa ni kupita kiasi na mimi napenda sana wakina mama wangekuwa wamejiunga kwenye hizi kozi tungekuwa tumepunguza sana ajalia”alisema Abiya Mpangile
Mkuu wa usalama barabarani Mkoa wa Njombe Jane Walioba amesisitiza madereva na wamiliki wa vyombo vya moto ikiwemo wa magari na pikipiki zote kujiunga na vyuo vya udereva kuepukana na changamoto za barabarani.
Kwa upande wao wahitimu wa udereva magari ya abiria waliofanya mtihani wao akiwemo Visent Stiven na Noa Kisaika wameahidi kuendesha magari yao kwa kuzingatia kanuni na sheria za barabarani na kushawishi wengine kujiunga na vyuo vya udereva ili kutokomeza matukio ya ajali.
“Kwanza ninashukuru kwa hii fursa hapa Njombe kwasababu miaka ya nyuma haikuwepo,nilivyoona hii fursa nimeona ni chachu ili kujua sheria kwa upana zaidi.Wito wangu kwa madereva ni kwamba tumemaliza mafunzo na tunanda kufanya kazi kwa vitendo kwa hiyo ni lazima tukawe watulivu kwasababu kila gari ina tabia zake”alisema Noa Kisaika
Abiya Mpangile Mkurugenzi wa chuo cha udereva Mpechi mjini Njombe.amesema fursa ya kupata mafunzo ya udereva wa magari ya abiria ameweza kuifikisha mkoani Njombe mara baada ya kutafakari shida za vijana wa Njombe wenye matamanio ya kuongoza vyomba vya kubeba abiria huku akiwataka madereva kuendelea kujitokeza kupata elimu ili kufikia ndoto zao.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment