Na Anthony Ishengoma
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Bi. Yasinta Mboneko amezindua mradi wa maji wa Mawaza- Negezi wenye thamani ya takribani bilioni 1.5 ambao utawanufaisha wakazi wapatao 15,429 wanaoishi katika vitongoji vinane vilivyoko nje kidogo ya Manispaa ya Shinyanga.
Bi. Yasinta Mboneko amezindua mradi huo leo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ujulikanao kama Mawaza -Negezi ulioko nje kidogo ya Maspaa ya Shinyanga ambao umefunguliwa katika maadhimisho ya Wiki ya Maji Mkoani Shinyanga.
Bi. Mboneko amewataka wasimamizi wa mradi huo ambao ni Mamlaka ya Maji Shinyanga SHUWASA kuhakikisha wafanyakazi wanaosimamia mauzo ya maji katika vizimba 27 vya mradi huo wasishindwe kutoa huduma ya maji kwa wananchi kwa visingizio vyovyote na endapo ikitokea wamepatwa na changamoto ya dharula basi awepo mbadala wa kufanya kazi hiyo.
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya ya Shinyanga amezitaka Mamlaka za maji Shinyanga na Taasisi nyingine Mkoani humo kuhakikisha zinazingatia sheria katika kulinda miundombinu ya maji pamoja na mazingira kwa miradi ambayo serikali inatumia fedha nyingi kuhakikisha inawanufaisha wananchi kwa ajili ya maendeleo kwa manufaa ya vizazi na vizazi.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Shinyanga Bw. Yusuph Matopola amesema kuwa awali mradi huo ulikadiliwa kupewa mkandarasi ambaye angetumia kiasi cha Tsh. Bil.3 lakini baada ya serikali kuanzisha mfumo wa akaunti ya dharula mradi huo mpaka kukamilika kwake utatumia takribani bilioni 1.4 na hivyo kuokoa kiasi kikubwa cha fedha kwani mpaka sasa SHUWASA ishatumia kiasi cha Tsh.Bil. 1.18 na mradi huo ushaanza kufanya kazi.
Wakati huo huo mwananzengo Bi. Mwatano Salum ameishukru Serikali kukamilisha mradi huo wa maji kwani wakazi wa eneo hilo kwa miaka mingi wamekuwa wakilazimika kwenda umbali mrefu kutafuta maji na wakati mwingine kukesha Kisimani wakitafuta maji au kuamka usiku wa manane kufuata maji hivyo mradi huo umekuwa mkombozi kwa jamii hiyo.
Aidha Bw.Lukasi Kulwa mkazi wa Mawaza Shinyanga aliongeza kuwa ukiachilia mabali kero ya maji kwa kipindi cha kiangazi ndoa za wakazi wa eneo hilo zilikuwa zikiingia mashakani kutokana na wanadoa wengi kupoteza muda mwingi wakifuatilia maji na hivyo kupunguza muda wa kujenga mahusiano yao.
Mradi huu Mwawaza –Negezi umezinduliwa katika wakati Taifa likiadhimisha wiki ya maji ambayo imeanza leo na kilele cha Wiki hii kitakamilika ifikapo mwezi Machi 22 ambapo miradi mbalimbali ya maji itazinduliwa katika Halmashauri mbalimbali za mkoa wa Shinyanga.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment