NMB yamkabidhi zawadi ya gutta Mshindi wa droo ya pili ya bonge la mpango | Tarimo Blog

 Raisa Said,Tanga

BENKI ya NMB kupitia kampeni yake ya Bonge la Mpango imekabidhi zawadi ya pikipiki ya miguu mitatu aina ya Lifan kwa mshindi wa droo ya pili ya kampeni hiyo Yusuph Kyando mkazi wa Mombo wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.

Pikipiki hiyo inagharimu shilingi milioni 4.4 ambapo tangu kuanza kwa kampeni hiyo mwezi Februari mwaka huu  zawadi zinazogharimu zaidi ya shilingi milioni 35.2 zimetolewa ikiwemo fedha taslimu na pikipiki sita za miguu mitatu aina ya Lifan.

Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi hiyo Meneja wa NMB kanda ya kaskazini Aikansia Muro alisema zaidi ya shilingi milioni 550 zimetengwa kwa ajili ya kampeni hiyo.

Alisema kuwa kampeni hiyo ni maalum kwa ajili ya kurejesha faida kwa wateja wa benki hiyo pamoja na kuhamasisha utamaduni wa kujiwekea akiba kwa watanzania.

" Tumelenga kuendeleza mazuri tuliyoyafanya mwaka 2020 mpaka tukaandika historia kubwa katika tasnia ya kibenki kwa kupata faida kubwa zaidi katika historia ya kibenki nchini",alisema Meneja huyo.

Alisisitiza kupitia kampeni hiyo zawadi zimekuwa zikitolewa kila wiki,mwezi na atatafutwa mshindi mmoja wa jumla atakatejishindia gari mpya aina ya Toyota Fortuner.

Muro alitaja zawadi zinazotolewa kuwa ni fedha taslimu kuanzia shilingi 100,000 mpaka 500,000,pikipiki aina ya miguu mitatu(Guta) aina ya Lifan na gari ya mizigo maarufu kama Kirikuu.

Kwa upande wake mshindi wa Bonge la Mpango  Yusuf Kyando alisema amefurahi kupata zawadi hiyo ambayo ataitumia kwa ajili ya kujiongezea kipato.

" Mimi nilijua ni maneno tu lakini leo ndiyo nimeamini kuwa ni kweli mimi ni mjasiriamali na zawadi hii imeniongezea kipato cha kukuza mtaji wangu kwa kweli nitaitumia kwa kujikwamua kiuchumi,",alisema Mshindi huyo.

Meneja wa NMB Tawi la Mombo Hamis Mwaduga alisema wataendelea kuhamasisha wateja kuweka fedha zao Benki ili waweze kunufaika na kampeni hiyo.

Naye Meneja wa NMB Tawi la Madaraka Tanga Elizabeth Chawiga alisema kuwa wamepata furaha kwa mshindi wa droo y ya pili ya Bonge la Mpango kutokea katika mkoa wa Tanga.

Hata hivyo katika droo ya tatu iliyofanyika jana washindi 11 wa kampeni ya Bonge la Mpango kutoka mikoa mbalimbali nchini wamejipatia fedha taslimu pamoja na washindi wawili wa pikipiki za miguu mitatu aina ya Lifan .





 



Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2