TAKUKURU SONGWE YAOKOA NYUMBA ILIYODHULUMIWA KWA MIKOPO UMIZA | Tarimo Blog

 


Mnamo tarehe 09.11.2020 Ofisi yetu ya TAKUKURU (M) Songwe ilipokea malalamiko yaliyohusu dhuluma ya nyumba aliyofanyiwa Ndg. JACOB MASEBO, nyumba iliyopo eneo la Mlowo, kiwanja Na.25. Dhuluma hiyo alifanyiwa na Ndg. RICHARD KALONGE mnamo mwaka 2009.

Katika taarifa hiyo, ilidaiwa kwamba mnamo mwaka 2009 Ndg. JACOB MASEBO alichukua mkopo kwa Ndg. RICHARD KALONGE kiasi cha Shs. 15,000,000/= na kukabidhi “Offer” ya hati nyumba yake kama dhamana ya mkopo husika. Kwa mujibu wa mkopo huo, Ndg. MASEBO alipaswa kulipa sh.33, 500,000 za mkopo huo pamoja na riba zaidi ya 50% na kwamba kama iwapo atashindwa kulipa fedha hiyo basi nyumba yake itakuwa mali ya Ndg. KALONGE. Kutokana na sababu hiyo, baada ya Ndg. MASEBO kushindwa kulipa mkopo kama walivyokuwa wamekubaliana, Ndg. KALONGE aliitaifisha nyumba iliyokuwa dhamana ya mkopo.

Baada ya Ofisi yetuya TAKUKURU Mkoa wa Songwe kupata taarifa, ilifanya uchunguzi na kubaini mambo yafuatayo:

  1. Kwamba ni kweli Ndg. JACOB MASEBO mnamo mwaka 2009 alikopa kiasi cha Shs. 15,000,000/= kwa riba ya 50% toka kwa Ndg. RICHARD KALONGE na dhamana ya mkopo huo ilikuwa ni nyumba yake ya biashara iliyopo Mlowo KIWANJA Na. 25.
  2. Kwamba nyumba ambayo hii ilikuwa na wapangaji ambao walikuwa wakilipa kodi kiasi cha Shs. 4,320,000/ kwa mwaka na mkopo huo alitakiwa kuwa amerejesha/ kulipa deni ndani ya siku nane.
  3. Baada ya Nd. MASEBO kushindwa kulipa mkopo ndani ya muda wa makubaliano, Ndg. KALONGE aliitaifisha nyumba iliyokuwa dhamana ya mkopo na kisha kubadilisha umiliki wa kiwanja na nyumba hiyo kutoka kwa Ndg. MASEBO kwenda kwenye umiliki wake katika Halmashauri yaWilaya ya Mbozi kupitia Ofisi ya Ardhi.
  4. Baada ya Ndg. KALONGE kubadilisha umiliki wa kiwanja, alitumia hati hiyo kuchukua mkopo benki ya CRDB na kukopa kiasi cha Shs.70, 000,000/= mkopo ambao tayari amemaliza kuulipa.
  5. Uchunguzi ulibaaini pia kuwa kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2010 hadi wakati Ofisi yetu inapokea taarifa hii, Ndg. KALONGE alikuwa akiipangisha nyumba aliyochukua kwa Ndg. MASEBO kwa Shs. 3,000,000/= kwa mwaka, hivyo kwa kipindi cha miaka 11aliweza kupokea kodi kiasi cha Shs. 33,000,000/=

Baada ya uchunguzi wa TAKUKURU mkoa wa Songwe kujiridhisha na kukubaliana na pande zote mbili, yafuatayo yalikubaliwa:

a)       Ndg. KALONGE aliridhia kubatilisha hati ya kiwanja alichojimilikisha toka kwa Ndg. MASEBO na kurejesha kiwanja hicho kwenye umiliki wa Ndg. MASEBO.

b)      Ndugu KALONGE aliridhia kugharamia gharama zote za mchakato wa kurejesha umiliki wa kiwanja hicho kwa Ndg. MASEBO.

c)      Pia Ndg. KALONGE alithibitisha kutomdai Ndg. MASEBO deni lake la Shs. 33,500.000/=  alilokuwa amemkopesha kufuatia kukiuka taratibu za kujimilikisha nyumba hiyo, kuchukua mkopo pasipo idhini ya mmiliki wa nyumba pamoja na kutumia nyumba yake kupangisha wapangaji na kuchukua kodi kwa kipindi cha miaka 11.

Kwa ushirikiano wa Ofisi ya Msajili wa Ardhi Mkoa wa Songwe, hati mpya ya umiliki wa kiwanja hicho cha Mlowo Na. 25 iliweza kuandaliwa kwa jina la mmiliki wa awali ambaye ni Ndg. JACOB EDMOND MASEBO.  Hati ambayo tayari amekabidhiwa.

NITOE WITO kwa wananchi wa mkoa wa Songwe kujiepusha na dhuluma ya aina hii na aina yeyote ile kwa wananchi wenzao. Serikali ipo na inafanya kazi. Haijalishi umedhulumu haki ya mtu mwingine kwa muda gani, tukipata taarifa tutaishughulikia na kuitatua.

 Tumejipanga vema kuhakikisha kuwa hakuna mwananchi yeyote yule anayeonewa na kudhulumiwa haki yake na mtu yeyote Yule ndani ya mkoa wetu. Nitoe wito kwa umma kutambua wajibu wao wa kutoa taarifa na kushirikiana na TAKUKURU katika mapambano haya kwa ustawi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Taifa letu.

 

Dkt. Damas Suta, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Songwe


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2