DK.HASSAN ABBAS ASHAURI WANAWAKE WALIOKO SEKTA YA HABARI NCHINI WAPEWE NAFASI | Tarimo Blog

Na Said Mwishehe, Michuzi TV 


KATIBU Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni ,Sanaa na Michezo Dk.Hassan Abbas amesema umefika wakati katika sekta ya habari wanawake wakaamiiwa na kupewa nafasi mbalimbali zikiwemo nafasi za Uhariri na nyingine zinazohitaji usimamizi.

Dk.Abbas ametoa kauli hiyo leo Aprili 28,2021 wakati akifungua semina ya wadau wa sekta ya habari iliyoandaliwa kati ya Wizara na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu na Sayansi(UNESC) jijini Dar es Salaam ikiwa na lengo la kutengeneza vipaumbele vya sekta hizo vitakavyoingia kwenye mipango ya kitaifa na kimataifa hasa katika utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Dunia(SDG's).

Pamoja na mambo mengine mengi yaliyozungumzwa na Dk.Abbas yakiwemo ya vyombo vya habari kujiimarisha kiuchumi, amezungumzia pia umuhimu wa waandishi wa habari wanawake kupewa nafasi na kuaminiwa kwenye sekta hiyo ya habari hasa kwa kuzingatia bado wengi wao wamekuwa hawapewi nafasi ukulinganisha na wanahabari wanaume.

"Wahariri wanawake ni wachache sana katika vyombo vya habari, ni kweli kuna mambo ya kihistoria kama ambavyo nimezungumza lakini nachofahamu histori ni kutukumbusha tulikotoka, tuliko na tunakokwenda lakini hii historia kwa upande wa wanawake walioko katika tasnia ya habari imesimama.Umefika wakati tukawaamini na kuwapa nafasi.

"Na katika hili naomba nizungumza na wamiliki wenzangu wa vyombo vya habari , unaweza kujiliuza mimi namiliki chombo kipi cha habari lakini, nami ni TBC na TSN, kwa upande wetu tumejitahidi, kule TSN kuna mwanamke ingawa amekaimu muda mrefu lakini tunashughulikia na tutawaweka mambo sawa na kwa upande wa TBC kule kuna mwanaume lakini anayemfuatia ni mwanamke,"amesema Dk.Abbass.

Amefafanua kuwa anatambua mchango wa wanawake kwenye sekta mbalimbali huku akitoa mfano yeye binafsi kwenye maisha yake wanawake wote ambao amekutana nao hawajawahi kumuungusha."Na hata mke wangu hajawahi kuniangusha".

Katika hatua nyingine,Dk.Abbas amesema licha ya wadau wa sekta ya habari kujadili masuala mbalimbali kwa lengo la kuboresha sekta hiyo ni vema wakakumbuka kujadili na kutafuta ufumbuzi za changamoto za kiuchumi kwani wadau wa habari wamekuwa wakijadili sana maslahi ya makundi mengine lakini ya kwao wamesahau.

"Mara chache sana tunapofanya semina na makongamano tunakumbuka kutathmini hili kwamba uhuru wa kiuchumi wa wanahabari ni muhimu sana, Mwanahabari ambaye analipwa kiduchu, hana uhakika wa mshahara, hana bima, hana pensheni kabla hajaenda kutafuta stori tayari hana uhuru" amesema.

Amesema kuna kila sababu ya wadau kujadili kuhusu changamoto hiyo ya kiuchumi na bahati nzuri wadau hao wanaelekea kwa Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari , hivyo ni wakati muafaka kujadili na mambo yanayohusu uchumi ndani ya tasnia hiyo."Wadau tumieni semina hii kuja na mapendekezo ya jinsi gani vyombo vya habari vitajiimarisha kimapato na uchumi".

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni ,Sanaa na Michezo Dk.Hassan Abbas(katikati) akifafanua jambo leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua semina ya wadau wa sekta ya habari iliyoandaliwa kati ya Wizara na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu na Sayansi(UNESC).Semina hiyo ilikuwa na lengo la kujadili na kutengeneza vipaumbele vya sekta hizo vitakavyoingia kwenye mipango ya kitaifa na kimataifa hasa katika utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Dunia(SDG's).Kulia ni Rose Reuben kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania(TAMWA) na kulia ni Mwakilishi kutoka UNESCO).
Katibu Mkuu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni ,Sanaa na Michezo Dk.Hassan Abbas(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa sekta ya habari waliokuwa meza kuu wakati wa semina hiyo iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Wadau sekta ya habari nchini wakiwa kwenye semina iliyoandaliwa na wadau wa sekta hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu na Sayansi(UNESC) kwa lengo la kujadili na kutengeneza vipaumbele vya sekta hizo vitakavyoingia kwenye mipango ya kitaifa na kimataifa hasa katika utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Dunia(SDG's).
Moja ya wahariri na wamiliki wa gazeti la Jamhuri Deodatus Balile akitoa mchango wake mbele ya Katibu Mkuu Wizara ta Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk.Hassan Abbas wakati wa semina iliyowakutanisha wadau wa sekta ya habari nchini.
Katibu Mkuu Wizara ta Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk.Hassan Abbas akiwa na baadhi ya wadau wa sekta ya habari walioshiriki semina hiyo.
Dk.Hassan Abbas ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo akimkabidhi tuzo kwa Mwandishi na Mtangazaji wa siku nyingi Penzi Nyamngumi wakati wa semina hiyo.
Mtangazaji wa siku wa RTD Edda Sanga akiwa na tuzo yake baada ya kuipokea leo ikiwa sehemu ya kutambua mchango wake katika tasnia ya habari nchini.
 

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2