"Ni wazi kwamba jina na Karume halitosahaulika katika ukombozi wa visiwa vya Zanzibar", Mheshimiwa Othman ameyasema hayo katika Kongamano la Kumbukumbu ya Rais wa Kwanza wa Visiwa vya Zanzibar, Hayati Mzee Karume, ambapo alimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Mheshimiwa Othman amesema kongamano hilo limefanyika ili kutoa fursa pia kwa wasomi na wananchi mbalimbali kutambua kikamilifu hekima, falsafa na fikra za kimapinduzi za kiongozi huyu shupavu zilizotokea katika historia ya taifa letu.
"Kwa kweli leo tuna heshima kubwa kuhudhuria kongamano hili lenye lengo la kuzienzi ndoto, fikra na falsafa za kiongozi huyu mweledi katika kuleta ukombozi wa nchi yetu. Karume ameiletea Zanzibar fahari kubwa sambamba na kuwafanya watu kuwa huru hata kujiamulia mambo yao wenyewe kwa uhuru na amani", alisema Makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Katika kusisitiza umuhimu wa kongamano hilo, Mheshimiwa Othman alisema ni dhahiri kwamba kongamano hili linawaleta waandishi na wasomi pamoja ili kupambanua kwa makini fikra na mchango wa Hayati Mzee Karume, ambapo mtu mmoja mmoja ataweza kuelewa kwa undani mambo aliyoyafanya kiongozi huyo wa kwanza wa Zanzibar na kuyaweka katika vitendo kwa ajili ya ujenzi wa taifa letu.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Bwana Steven Wasira, amesema shabaha ya kongamano hilo ni kurithisha historia kutoka kizazi kimoja kwenda chengine.
"Tuna mengi ya kujifunza kwa Karume, kwani alikuwa ni miongoni mwa viongozi wakuu wa bara la Afrika kudai uhuru wa nchi zao pamoja na bara la Afrika kwa ujumla," amesema Bwana Wassira.
Kongamano hilo ambalo lilihudhuriwa na viongozi, wafanyakazi na wanafunzi kutoka katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere pamoja na wageni waalikwa limefanyika katika chuo hicho kilichopo Bububu, nje kidogo ya mji wa Unguja.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment