Mufti Mkuu wa Tanzania Shehe Aboubakary Zubeiry ameipongeza BancABC Tanzania ambayo ni kampuni tanzu ya Atlas Mara kwa kuunga mkono mikakati ya Serikali ya kuongeza tija katika sekta ya huduma za fedha na kupanua huduma hizo ili kuwafikia watanzania walio wengi na ambao hawajafikiwa na huduma za kibenki.
Shehe Zubeiry aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akiongea na wateja pamoja na wafanyakazi wa BancABC Tanzania wakati wa futari iliyoandaliwa na benki hiyo kwa wateja wake.
‘Naomba niwapongeze sana BancABC kwa juhudi zenu kubwa mnazo weka kwenye kupanua huduma zenu ili kuwafikia Watanzania walio wengi na hasa kwenye maeneo ya vijijini. Hii ni hatua kubwa sana na ya kupongezwa kwani kadri mnavyoendelea kuwafikia Watanzania wengi ndipo mnapozidi kuwafungulia milango ya kujiongeza kiuchumi na hivyo kuunga mkono juhudi za serikali za kuongeza kipato kwa wananchi wake,’ Shehe Zubeiry alisema.
‘Nimepata taarifa kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji kuwa BancABC pia imekuwa ikishiriki katika utekelezaji wa masuala ya kijamii. Mkurugenzi amesema kuwa kwa kushirikiana na Wizara ya Afya wakati wa Mheshimiwa Ummy Mwalimu kwenye kutoa huduma ya bima ya afya kwa Watoto yatima, kushirikiana na Taasisi ya Mheshimiwa Stella Ikupa katika kukuza uelewa wa huduma jumuishi za kifedha kwa watu wenye ulemavu pamoja na kushirikiana na TAMISEMI katika ujenzi wa vyoo na vyumba vya madarasa ya shule mbalimbali nchini. Hii ni ishara tosha kuwa BancABC ni mshirika mzuri katika masuala ya jamii na wanapongeza kwa hilo na kuwaomba kwa Mungu azidi kuwapa nguvu ya kuzidi kufanya Zaidi ya hayo,’ Mufti Mkuu huyo wa Tanzania alisema.
Awali, wakati akimkaribishwa Mufti Mkuu, Mkurugenzi Mtendaji wa BancABC Tanzania Imani John alisema kuwa BancABC inatoa huduma mbalimbali kwa watu binafsi, wajasiriamali wadogo na wa kati pamoja na wateja wakubwa zikiwemo huduma za kuweka fedha pamoja na mikopo wezeshi kwa wateja wa madaraja yote.
Kwa kipindi ambacho tumekuwa tukitoa huduma, ubunifu wa huduma za BancABC pamoja na mipango yetu madhubuti imepelekea kutambuliwa na wadau mbalimbali katika sekta ya huduma za kifedha na imetupatia tuzo mbalimbali.
Na kwa kudhihirisha ubora wa ubunifu wa huduma zetu, BancABC Tanzania iliweza kushinda tuzo ya ‘the Most Emerging Bank in East Africa through the Banker Africa – East Africa Awards’ yaani (Tuzo ya benki inayokua kwa haraka Afrika Mashariki) kwa Tuzo za Afrika Mashariki – ambazo zilifanyika jijini Nairobi kwa miaka miwili mfululizo – 2017 na 2018. Hili ni jambo la kujivunia na tunahidi kuendelea kutoa huduma zenye ubora wa juu kwa lengo la kukidhi mahitaji ya wateja wetu, alisema John.
Aliongeza kuwa BancABC inazo huduma za kadi za malipo ya kabla, ambazo ni maalum kwa wateja kufanya miamala bila ya kuwa na akaunti kwa njia salama na nafuu kwa malipo ya njia ya mtandao na kwenye mashine za malipo yaani “POS machines” ambazo zimetambuliwa na kupewa tuzo na VISA kwa miaka mitatu mfululizo.
‘Tuzo hizo zinazojulikana kama “Leading in e-Commerce transactions Award” zinamaanisha kuwa kadi zetu zinaongoza nchini katika malipo ya mtandaoni’, alisema John huku akiongeza kuwa kadi hizi zinapatikana katika sarafu sita tofauti ambazo ni Shilingi ya Tanzania, Dola ya Kimerakani, Randi ya Afrika ya Kusini, Pauni ya Uingereza, Yuro ya Ulaya pamoja na Yuan ya China.
Mkurugenzi Mtendaji wa BancABC Tanzania Imani John (kulia) akimkabidhi kadi ya malipo ya kabla Mufti Mkuu wa Tanzania Shehe Aboubakary Zubeiry wakati wa futari iliyoandaliwa na benki hiyo kwa wateja wake jana jijini Dar es Salaam.
Mufti Mkuu wa Tanzania Shehe Aboubakary Zubeiry akiongea na wateja wa benki hiyo pamoja na wageni waalikwa wakati wa futari iliyoandaliwa na benki hiyo kwa wateja wake. BancABC Tanzania iliandaa futari ikiwa ni ishara ya kuonyesha upendo na kujali hasa kwa wale ambao wako kwenye mfungo kwa kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Mkurugenzi Mtendaji wa BancABC Tanzania Imani John akiongea na wateja wa benki hiyo pamoja na wageni waalikwa wakati wa futari iliyoandaliwa na benki hiyo kwa wateja wake. BancABC Tanzania iliandaa futari ikiwa ni ishara ya kuonyesha upendo na shukurani hasa kwa wale ambao wako kwenye mfungo kwa kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment