SERIKALI imeahidi kuchukua hatua kali kwa mfanyabiashara yoyote atakaebainika kupandisha bei za bidhaa au huduma kwa utashi ama tamaa bila ya kuwepo sababu ya msingi kwani tayari imeshatoa bei elekezi za bidhaa muhimu za chakula.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema hayo leo katika risala yake aliyoitoa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari ya kuukaribisha mwezi Mtukufu wa Ramadhan mwaka huu 2021 Miladia sawa na mwaka 1442 Hijria.
Katika risala yake hiyo, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kwamba kwa pamoja ni vyema wananchi wenye kipato cha chini wakafikiriwa hasa katika kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambapo mahitaji ya familia yanaongezeka.
Alisisitiza kwamba kwa msingi huo huo, wafanyabiashara wa bidhaa zote zikiwemo za nguo ni vyema wakazingatia uwezo wa wananchi kwani kuwakatia nguo watoto katika kipindi hichi kwa ajili ya Sikukuu ni sehemu ya utamaduni wa wananchi wote wa Zanzibar.
Aliongeza kuwa inafurahisha kuona kwamba licha ya kuwepo kwa changamoto za usafirishaji na upatikanaji wa biadhaa mbali mbali, shughuli za biashara na upatikanaji wa chakula hapa nchini zinaenda vizuri ambapo bidhaa zote muhimu zinapatikana wakati huu mwezi wa Ramadhani ukikaribishwa.
Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa taarifa za Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo inatoa matumaini ya kuwepo kwa chakula cha kutosha yakiwemo mazao ya muhogo na ndizi ambayo hutumiwa na wananchi wengi kwa futari katika mwezi wa Ramadhani.
Aidha, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa mnamo Machi 04 2021 alikutana na wafanyabiashara wakubwa wanaoingiza chakula na kuwataka washirikiane na Serikali kufanya maandalizi mazuri katika kuhakikisha kwamba bidhaa zote hasa za chakula kwa wananchi wa Zanzibar ziweze kupatikana katika kipindi chote cha mwezi wa Ramadhani na baada ya hapo.
Alhaj Dk. Mwinyi alieleza kwamba kwa hakika ibada ya Saumu ina mchango mkubwa katika kuimarisha uchamungu, jambo ambalo ni jema na linaleta manufaa hapa Duniani na kesho Akhera.
“Kwa hivyo, tuukaribishe Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa furaha na matumaini na tujiandae kunufaika kutokana na neema na fadhila mbali mbali zilizo katika kipindi chote cha Mwezi huu tunaoukaribisha”, alisema Alhaj Dk. Mwinyi.
Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Mwinyi aliwaomba Waumini wa Dini ya Kiislamu kuhimizana kutekeleza ibada za Faradhi sambamba na kukithirisha ibada za Sunna ili kupata radhi za Mola ambapo miongoni mwa ibada iliyosisitizwa zaidi kufanywa kwa wingi katika mwezi wa Ramadhani ni kusoma Qur-an tukufu.
Alieleza kwamba katika kutafuta fadhila za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani imehimizwa kujitahidi sana kutekeleza ibada ya sala zote za Faradhi na sala za Sunna, kuomba dua, kusoma nyiradi mbali mbali, kufanya itikafu, na kutekeleza Sunna nyengine zinazoambatana na Mwezi wa Ramadhani.
Aliongeza kwamba jambo jengine linalohimizwa kutekeleza zaidi ndani ya Mwezi wa Ramadhani ni kutoa sadaka hasa kwa watu wenye mahitaji, Mayatima, Wazee, Masikini na Mafakiri ibada ambayo inaongeza baraka na mahusiano mema katika jamii.
Alhaj Dk. Mwinyi pia, alitumia fursa hiyo kuwahimiza wananchi pamoja na viongozi na Watumishi wa Manispaa zote nchini juu ya umuhimu wa kuzingatia usafi katika miji hasa katika masoko na maeneo yanayohusika na uuzaji wa vyakula ili kujiepusha na maradhi ya mripuko.
Kadhalika, aliwahimiza viongozi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kuhakikisha huduma za maji zinawafikia wananchi hasa katika maeneo ambayo huduma hiyo haipatikani kwa uhakika.
Aliwataka Masheha wa Shehia ambazo zina matatizo ya maji wawasiliane na (ZAWA) ili kuhakikisha hatua zinachukuliwa zikiwemo kuwapelekea wananchi magari ya maji kwa lengo la kuondokana na usumbufu wa kupata huduma hiyo.
Sambamba na hayo, Alhaj Dk. Mwinyi aliwahimiza viongozi wa Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani pamoja na Jeshi la Polisi kuhakikisha wanasimamia ipasavyo sheria za usalama barabarani wakati wote na kuongeza nguvu hasa katika kipindi hiki ambacho mahitaji ya usafiri huongezeka.
Aliwataka kuwachukulia hatua kali za kisheria madereva watakaojaribu kuvunja sheria za usalama barabarani kwa kwenda mwendo wa kasi pamoja na wale wenye tabia ya kuwasumbua wananchi kwa kuwashusha bila ya kuwafikisha mwisho wa vituo vilivyopangwa na Serikali.
Hata hivyo, Alhaj Dk. Mwinyi aliwakumbusha wananchi wenye dharura maalum na wale wasiokuwa Waislamu waendeleze utamaduni wa kujizuia kula hadharani, kutovaa nguo zisizoendana na maadili ya Kizanzibari sambamba na kuepuka matendo yatakayowakwaza Waislamu wenye kutekeleza ibada ya funga.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment