Na Mwandishi wetu, Globu ya Jamii
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa mradi wa reli ya kisasa wa SGR utaendelea kujengwa mpaka ukamilike kwa awamu ya kwanza yote kwani fedha zote zimeshalipwa kwa kampuni inayojenga.
Hayo ameyasema wakati akagua jengo la Stesheni ya Reli ya Kisasa ya SGR Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Daraja la KM 2.56 linalounganisha Stesheni hiyo lililopo eneo la Kariakoo. Amesema kuwa mradi wa Reli ya kisasa umegawanyika katika awamu tatu mpaka ukamilike na mpaka sasa umekamilika kwa asilimia 91 kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro.
Na asilimia 60 umeshakamilika kutoka Morogoro mpaka Dodoma huku mafundi wa ujenzi wa reli hiyo wakiwa kazini kwa masaa 24 kwa wiki.
Akitembelea Jengo la Tanzanite lililopo Stesheni mkoa wa Dar es Salaam amesema kuwa kituo hicho kimeshakamilika na kinauwezo wa kuchukua watu 3200 kwa mara moja kwani jengo hilo lina ghorofa tatu na kutakuwa kunafanyika shughuli mbalimbali ambazo ni fursa kwa watanzania.
"Makampuni yote yanayojenga kama Yapi Merkenzi mpaka hapa tulipo tumeshawalipa mpaka hatua ya mwisho ya 'Certificate' (Cheti) waliyotuletea na tumejipanga vizuri wakileta 'Certificate' tutalipa. Amesema Majaliwa.
Waziri Mkuu amesema kuwa taarifa ya Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Reli (TRC) imetupa faraja kwamba 'kuanzia mwezi wa nane tunaanza kuungulimisha treni yetu ya umeme kuanzia Morogoro kuja Dar es Salaam' lakini itaishia Pugu na baadae itafika Stesheni pale ujenzi utakapokamilika." Amesema Majaliwa.
Hata hivyo waziri Mkuu amewatoa wasiwasi watanzania kuhusu umaliziaji wa miradi mikubwa iliyopo hapa nchini kuwa itamalizika kama ilivyopangwa na kutoa huduma kwa watanzania.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania, Masanja Kadogosa amesema mradi wa Reli ya kisasa utaanza kufanya kazi kuanzia Agosti, 2021 utaanza kufanya kazi kuanzia Kituo cha Morogoro Mpaka Pugu na kutoka Pugu treni ndogo itatumika kutoka Pugu mpaka Stesheni.
Kadogosa amesema kuwa Ujenzi wa Reli ya kisasa unaendelea vizuri. "Kuna makaravati zaidi ya 248 yameshakamilika, madaraja 117 yamekamilika, ujenzi wa tuta la Reli umeshakamilika. Lakini ukiachana na Urefu wa kutoka Dar es Salaam mpaka pugu, kuna sehemu yenye urefu kilimita 193 ambayo bado haijakamilika."
Hata hivyo Kadogosa amebaisha kuwa kunabaadhi ya mabehewa na vichwa vya Reli ya kisasa vitakuwa vimeshawasili hapa nchini katikati ya Julai, 2021 kwaajili ya majaribio mara baada kukamilika kwa ujenzi wa reli kutoka Pugu kwenda Morogoro.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania, Masanja Kadogosa akitoa maelekezo wakati Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa alipotembelea kituo cha Tanzanite kilichopo Stesheni mkoani Dar es Salaam.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akioneshwa mashine za kielektroniki za tiketi katika kituo kikuu cha reli ya mwendo kasi (Tanzanite) na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, wakati alipokagua kituo hicho Aprili 20, 2021, jijini Dar es salaam
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, wakati alipokagua kituo kikuu cha reli ya mwendo kasi (Tanzanite) , jijini Dar es salaam Aprili 20, 2021.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akioneshwa picha iliyotengenezwa kwa mawe maalum kwenye ukuta wa mapokezi katika kituo kikuu cha reli ya mwendo kasi (Tanzanite) na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, wakati alipokagua kituo hicho Aprili 20, 2021, jijini Dar es salaam.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment