MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amewakabidhi rasmi wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Mkoa wa Ruvuma tuzo waliopewa baada ya kuvuka malengo ya ukusanyaji kwa asilimia 114.
Akizungumza kabla ya kukabidhiwa tuzo hiyo katika hafla iliyofanyika ukumbi wa TRA mjini Songea,Meneja wa TRA mkoani Ruvuma Amina Ndumbogani amesema katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Machi 2021 wamefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 13 kati ya lengo la kukusanya zaidi ya sh.bilioni 12.
“Tumeweza kuvuka malengo yaliyowekwa katika kipindi cha Julai 2020 hadi Machi 2021 kwa asilimia 110,makusanyo hayo ni ongezeko la asilimia 11’’,alisema Ndumbogani.
Hata hivyo Meneja huyo ameyataja makusanyo ya ya kodi ya ndani katika kipindi hicho yalikuwa ni zaidi ya shilingi bilioni 13 na kuvuka lengo la zaidi ya shilingi bilioni 11 hivyo kuvuka lengo kwa asilimia 114.
“Tunapenda leo utukabidhi rasmi tuzo ya ngao ya ushindi tuliopewa Arusha Januari mwaka huu baada ya kuvuka malengo ya kipindi cha miezi sita,kuanzia Julai hadi Desemba 2020’’,alisema.
Amesema kwa mwezi Machi mwaka huu,TRA Ruvuma ililenga kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 1.417 ambapo makusanyo halisi yalifikia zaidi ya shilingi bilioni 2.356 sawa na asilimia 166.
Akizungumza baada ya kukabidhi tuzo hiyo,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amewapongeza TRA kwa kufanyakazi kwa ufanisi mkubwa hali iliyosababisha kuvuka malengo ya ukusanyaji mapato.
“Tuzo mliopewa ni heshima kwa TRA na wadau wa kodi wa Mkoa wa Ruvuma,tuzo hii inaonesha namna mlivyotambulika kitaifa,tuzo hii iwe chachu ya kuongeza bidii ili kuvuka malengo ya matarajio ya serikali’’,alisisitiza Mndeme.
TRA ilianzishwa mwaka 1996 kupitia sheria namba 11 ya mwaka 1995 ikibainisha majukumu yake makubwa kuwa ni kukadiria,kukusanya na kuhasibu mapato yote ya serikali kuu.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment