USHIRIKA UWE NA MASHAMBA YA UZALISHAJI KOROSHO – RC BYAKANWA | Tarimo Blog

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa ametoa wito kwa Ushirika kuangalia namna bora ya kuongeza uzalishaji wa zao la Korosho kwa Vyama vya Ushirika kuwa na maeneo ya mashamba yao ya uzalishaji wa Korosho.

Mkuu wa Mkoa Byakawa ameyasema hayo leo Aprili 21, 2021 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 21 wa Chama Kikuu cha Masasi, Mtwara Cooperative Union (MAMCU), katika Chuo cha Ualimu Mtwara.

Akiongea wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mkoa amewataka viongozi wa Vyama vya Ushirika kuwa na maono makubwa yenye uendelevu wa zao la Korosho utakaosaidia kilimo hicho kuwa endelevu na kuongeza uzalishaji wa Korosho.

“Ili tuwe na zao endelevu lenye uhakika na usalama wa uzalishaji lazima ushirika uwe na mashamba yao ya Korosho ardhi haiongezeki, hivyo tuangalie namna bora ya kutumia mapori na ardhi isiyotumika kwa kufuata taratibu zilizopo kuongeza mashamba ya Korosho,” alisema Mkuu wa Mkoa

Mkuu wa Mkoa huyo alieleza kuwa ni wakati sasa kwa wakulima wa Korosho kuwajibika katika kuhakikisha kuwa uzalishaji wa zao hili unaongezeka kwa kufuata kanuni za Kilimo bora kama vile matumizi ya mbegu bora, umbali wa mikorosho shambani, kujua tabia na utunzaji sahihi wa mikorosho.

“Wakulima wengi mmerithi mikorosho ya miaka mingi isiyozaa na pengine hamjui hata alipanda nani, mnaachia mapori kuchanganyika na mikorosho, hamtumii mbinu za kisasa za Kilimo, niwaombe sana tubadilike,” alisema RC Byakanwa

Aliongeza kuwa wakulima wa Korosho wanaweza kuleta mapinduzi chanya ya kilimo cha Korosho kwa wakulima kuamua kuchukua hatua stahiki za kuwajibika na kilimo chao wenyewe kabla ya kuangalia changamoto nyingine.

Moja ya ajenda kuu za Mkutano huo ni pamoja na uchaguzi wa Viongozi wa Wajumbe wa Bodi wa pamoja na Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika MAMCU. Hivyo, RC Byakanwa amewataka wajumbe wa Mkutano huo kuchagua viongozi waadilifu, wanaoweza kusimamia Ushirika kwa kuwa na elimu, viongozi wenye maono na mikakati ya kuendeleza Chama na Ushirika kusonga mbele.

“Tumieni haki na demokrasia yenu vizuri kwa kuchagua Viongozi wenye sifa, viongozi wenye maadili na uadilifu mkubwa msichague viongozi ambao baada ya siku chache watatuingiza kwenye migogoro,” alisisitiza RC Byakanwa

RC Byakanwa amepongeza miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa na Chama Kikuu cha Ushirika MAMCU ikiwa ni pamoja na maghala ya yanayojengwa ikiwemo ghala la Ndwika Wilayani Nanyumbu Halmashauri ya Masasi, ghala la Ntimbwilimbwi Wilaya ya Nanyamba Halmashauri ya Mtwara.

Akisoma taarifa ya Mwenyekiti anayemaliza muda wake wa Uongozi wa MAMCU Joseph Kidando ameeleza Chama Kikuu cha Ushirika MAMCU Ltd kinahudumia wakulima kutoka maeneo ya Nanyumbu, Masasi Mji, Masasi Vijijini, Mtwara Mji, Mtwara Vijijini pamoja na Halmashauri ya Nanyamba chenye wanachama Vyama vya Ushirika vya Msingi vipatavyo 164 mkoani Mtwara. Alibainisha kuwa Shughuli kuu za Chama hicho ni pamoja na Usimamizi, uhifadhi na utafutaji wa masoko ya mazao ya Wakulima Mkoani Mtwara. 

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa akifungua Mkutano Mkuu wa 21 wa Chama Kikuu cha Ushirika MAMCU Ltd kilichofanyika Aprili 21, 2021 katika Chuo cha Walimu Mkoani Mtwara.

 Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika Bw.Collins Nyakunga akifafanua jambo wakati wa Mkutano Mkuu wa 21 wa Chama Kikuu cha Ushirika MAMCU Ltd kilichofanyika Aprili 21, 2021 katika Chuo cha Walimu Mkoani Mtwara

Mrajis Msaidizi wa Mkoa wa Mtwara Bw. Juma Mokili akieleza taratibu na Kanuni za Ushirika Mkutano Mkuu wa 21 wa Chama Kikuu cha Ushirika MAMCU Ltd kilichofanyika Aprili 21, 2021 katika Chuo cha Walimu Mkoani Mtwara.

 


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2