Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akimsikiliza Meneja Mradi kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC) anayesimamia Sehemu ya Makutupora-Morogoro, Mhandisi Mateshi Tito, akimweleza namna mashine ya kuunganisha mataruma inavyofanya kazi katika ujenzi wa reli ya Kisasa ya SGR, wilayani Kilosa, Mkoani Morogoro., mwishoni mwa wiki.
Meneja Mradi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) anayesimamia Sehemu ya Makutupora-Morogoro, Mhandisi Mateshi Tito, akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, nati za kufungia mataruma, wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea mradi wa ujenzi wa reli ya Kisasa ya SGR, Wilayani Kilosa, Mkoani Morogoro.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akiangalia sehemu ya mataruma iliyoungwa katika reli ya kisasa ya SGR, sehemu ya Makutupora hadi Morogoro, wilayani Kilosa, Mkoani Morogoro, alipokagua maendeleo ya ujenzi wake, mwishoni mwa wiki.
Mmoja wa mafundi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), akifunga nati katika mataruma, katika kiwanda cha Mataruma kilichopo Igandu, Wilayani Mpwapwa, Mkoani Dodoma, mwishoni mwa wiki.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akimsikiliza Mtaalam wa Maabara katika kiwanda cha Mataruma Kelvin Kimaro, akimweleza kuhusu ubora wa mataruma, wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea kiwanda hicho kilichopo Igandu, Wilayani Mpwapwa, Mkoani Dodoma.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akizungumza na wafanyakazi wa Kampuni ya Yapi Merkezi inayojenga Reli ya Kisasa ya SGR Sehemu ya Morogoro- Makutupora, wilayani Kilosa, Mkoani, wakati Naibu alipotembelea kiwanda hicho kilichopo Igandu, Wilayani Mpwapwa, Mkoani Dodoma.
……………………………………………………………………………………….
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara amewataka wananchi wa Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro kuhakikisha wanatumia fursa ya ujenzi wa Reli ya Kisasa ya (SGR) kujiimarisha kiuchumi kwa kuongeza uaminifu katika utendaji kazi wakati wa ujenzi.
Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya Ujenzi wa reli hiyo Sehemu ya Makutupora hadi Morogoro (KM 422), Naibu Waziri Waitara amesema kuwa uaminifu wao katika mradi huo utapelekea kuwea kupata fursa kwa wao kuajiriwa kama wafanyakazi baada ya mradi kukamilika.
“Mradi huu ni wa kihistoria na ninyi mmepata ajira hapa, tumieni fursa hii vizuri kwani mkifanya kazi hii kwa uaminifu, mradi unaweza kukamilika na mkapata ajira ya moja kwa moja kwenye shirika la reli” amesisitiza Naibu Waziri Waitara.
Aidha, Naibu Waziri Waitara amemtaka Mkandarasi kuhakikisha anazingatia viwango vilivyowekwa kwenye mkataba ili mradi huo uweze kuwa na matokeo chanya kama ilivyokusudiwa.
Ameongeza kuwa kwa changamoto yoyote inayojitokeza lazima watendaji na wafanyakazi waziripoti kwa wakati na kwenye vyombo sahihi ili zisikwamishe mradi kukamilika.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amesema mpaka sasa sehemu ya Makutupora hadi Dodoma imefikia asilimia zaidi ya 55 na kumuhakikishia Naibu Waziri kusimamia mradi huo kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa kwenye mkataba.
Kadogosa amesema kuwa mpaka sasa suala la wafanyakazi limezingatia mkataba kwa kuwa na wafanyakazi wazawa asilimia 88 na wafanyakazi kutoka nje asilimia 12 na kusema kuwa shirika linaendelea kupata ujuzi utakaopunguza gharama kubwa za kuwarudisha wataalam kutoka nje mara baada ya mradi kukamilika.
Naye Meneja Mradi wa TRC Sehemu ya Makutupora hadi Morogoro, Mhandisi Mateshi Tito amesema kuwa licha ya uwepo wa changamoto za mara kwa mara ikiwemo mvua zinazoendelea kunyesha bado kazi ya ujenzi inaendelea vizuri na TRC imejipanga kutatua changamoto zozote zitakazojitokeza.
Mradi wa reli ya Kisasa ya SGR kuanzia Dar es Salaam hadi Mwanza wenye jumla ya Kilomita 1912, unatekelezwa kwa awamu tano ambazo ni pamoja na Dar es Salaam hadi Morogoro KM 300, Morogoro hadi Makutupora KM 422, Makutupora hadi Tabora KM 371, Tabora hadi Isaka KM 162 na Isaka hadi Mwanza KM 349 ambapo mpaka sasa Sehemu ya Dar-Moro, Moro-Makutupora na Isaka-Mwanza wakandarasi wanaendelea na mradi.
(Imetolewa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.)
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment