Wananchi Mtwara washutumiwa kukata nyaya za umeme na kuvulia samaki aina ya pweza | Tarimo Blog

Na ANNE ROBI, Mtwara .


SHIRIKA la Umeme mkoani Mtwara TANESCO), limewataka viongozi wa kata na vijiji vilivyopo kando kando ya bahari kuhakikisha wananchi wa maeneo yao wanaacha tabia ya kuharibu miundombinu ya umeme na kusababisha kukatika kwa nishati hiyo mara kwa mara.

Afisa Uhusiano na huduma kwa wateja TANESCO Mtwara Jumanne Mkunguu alitoa wito huo jana na kusema kuwa miongoni mwa sababu za kukatikakatika umeme katika vijiji hivyo ni kukatwa kwa nyaya za kushikia nguzo za umeme na kutumiwa  kuvulia samaki aina ya pweza.

“Taarifa ambazo tunazo zinasema kwamba wananchi wa maeneo ya vijiji na kata zinazopakana na bahari wanakata nyaya za kushikia nguzo kwa ajili ya kukata vyuma vya kuvulia samaki aina ya pweza,” amesema na kutoa wito kwa viongozi wa maeneo hayo kuhakikisha wananchi hao wanaacha mara moja kuharibu miundombinu ya umeme na kusababisha kukakatika mara kwa mara.

Mkunguu amesema tatizo la kukatikakatika umeme ni kubwa katika vijiji vya kandokando ya bahari. Ametaja baadhi ya maeneo yenye tatizo kubwa la kukatikakati umeme kuwa ni MsangaMkuu, Msimbati na Naumbu

“Kwa mfano tulienda kijiji cha Mgao ambao wamekosa umeme kwa siku nne na moja ya sababu kubwa inayotajwa ni kukatwa kwa nyaya za umeme na kusababisha nguzo kuanguka. Niwasihi viongozi wahakikishe wananhci wanalinda miundombinu ya umeme kwa sababu shirika la umeme ni shirika la umma ambapo na wao ni wahusika,” amesema.

Afisa huyo alisema wakati wa ziara ya maafisa wa shirika hilo kutoka ofisis ya Mtwara walipo tembelea baadhi ya maeneo ambayo yamekuwa yanakumbwa mara kwa mara na tatizo la kukatika umeme.

Wakiongea wakati wa ziara hiyo baadhi ya viongozi wa kata walikili kuwepo kwa tatizo la kukata nyaya za umeme huku wakilitaka shirika la TANESCO kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kujua umuhimu wa miundombinu ya umeme katika maeneo yao.

Mtendaji wa kata ya Naumbu Kaiza Mnete alikiri kuwepo kwa changamoto ya kukatwakatwa kwa nyaya za kushikia nguzo za umeme katika vijiji vya kata hiyo huku akisema tatizo ni wananchi kukosa elimu kuhusu umuhimu wa miundombinu ya umeme katika maeneo yao.

“Ni kweli hiyo changamoto ipo na sisi tulishajiridisha kwamba kuna nguzo ambazo nyaya zake ambazo hushikilia nguzo zimekuwa zikikatwa na kusababisha kata hiyo kupata umeme ambao sio wa uhakika kila mara,” amesema.

Amesema kamati ya ulinzi na usalama katika kata hiyo imekuwa ikichukua hatua kuhakikisha miundombinu ya umeme inalindwa huku akisisitiza umuhim wa shirika hilo kutoa mafunzo kwa kata hiyo ili wananchi waelewe umuhimu wa kushiriki katika kutunza miundombinu hiyo.

“Tunafaham wananchi ndio wanaohujumu hiyo miundombinu bila kujali kwa sababu huwa wanahujumu kwa ajili ya manufaa yao binafsi, zile nyaya zinakatwa kwa ajili ya matumizi ya uvuvi bila kujali kwamba wanapokata zile nyaya wanasababisha hasara kwa shirika na kukosesha wenzao hudumu ya umeme,” amesema.

Amesema wananchi hawatoi ushirikiano katika kuwabaini wanaokata hivyo na kurudisha nyuma harakakati za kuwakamata wanaohujumu hiyo miundombinu.

Baadhi ya wavuvi walikana kutumia nyaya za umeme katika kuvulia samaki huku wakiahidi kutoa ushirikiano kwa shirika hilo katika kuwabaini wanaotumia nyaya hizo za umeme kuvulia samaki.

“Mimi ninachoona ni kushirikiana na TANESCHO kwa ajili ya kubaini hilo kama ni kweli basi wale wanaohusika wachukulie hatua, ila kwa mimi situmii hizo nyaya katika uvuvi wangu,” amesema Ally Mohammed mvuvi wa kata ya Mgao Halmashauri ya Mtwara.

Baadhi ya nyaya za umeme zikiwa zimening'nia baada ya kukatwa na wananchi ambao inasemakana wanazitumia Kwa ajili ya kuvulia samaki aina ya pweza


Maafisa wa shirika la umeme TANESCO Mtwara wakikagua baadhi ya miundombinu ya umeme ambayo nyaya zake za kushikia miti ya umeme umekatwa na wananchi Kwa ajili ya kutumia katika uvuvi wa samaki aina ya pweza
 

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2