Mwakilishi wa Balozi wa Japan nchini, Bw. Niinuma Takashi, akimsikiliza Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (hayupo pichani), wakati wa mkutano katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.
Na. Josephine Majura, WFM, Dodoma
Wizara ya Fedha na Mipango imepokea na kuanza kuyafanyia kazi maagizo ya Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan, kuhusu misamaha ya kodi kwa fedha za misaada ili kutekeleza miradi ya vipaumbele.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi wa Balozi wa Japan nchini, Niinuma Takashi, ambaye alilalamikia suala la kodi kwa fedha za mikopo na misaada inayotolewa na nchi hiyo.
Dkt. Nchemba alieleza kuwa Mhe. Rais ametoa maagizo hayo kwasababu fedha za msaada zikitolewa kwa ajili ya kusaidia jamii na hata zikitozwa kodi pia kodi hiyo itatumika kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya nchi na wananchi kwa ujumla.
“Hili jambo tunalifanyia kazi na mpaka sasa tumeshaandaa waraka na tunasubiri ratiba ya Baraza la Mawaziri kwa ajili ya kuupitisha katika baraza hilo ili ukidhi matakwa ya kisheria”, alisema Dkt. Nchemba.
Alimuhakikishia Mwakilishi wa Balozi huyo kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na Japan katika nyanja mbalimbali kwa maendeleo ya nchi zote mbili.
Naye Mwakilishi wa Balozi wa Japan nchini Tanzania, Niinuma Takashi, aliahidi kuwa nchi yake iko tayari kuendeleza uhusiano na ushirikiano na Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kutoa misaada ya kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya vipaumbele ikiwemo bandari ya Kigoma na mradi wa maji Zanzibar.
Aliongeza kuwa endapo changamoto ya misamaha ya kodi itaondolewa kwenye fedha za misaada na mikopo inayotolewa, uhusiano wa Tanzania na wadau wa maendeleo utazidi kuimarika na kubainisha kuwa nchi yake ipo tayari kupokea maombi mapya ya kufadhili miradi mipya ya kipaumbele.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment