Shirika la Viwango Tanzania (TBS), limeendelea na zoezi la kusajili majengo ya chakula na vipodozi katika Halmashauri za wilaya ya Mlimba na Ulanga mkoani Morogoro ambapo zaidi ya majengo 140 yamesajiliwa katika maeneo hayo.
Usajili huu wa majengo ya chakula na vipodozi unaenda sambamba na ukaguzi bidhaa katika majengo na maduka pamoja na kutoa elimu kwa wafanyabiashara hao.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo Afisa Udhibiti Ubora wa TBS, Bw. Daniel Kahabi amesema Shirika limejikita katika kuhakikisha linafika katika pande zote za nchi na kufanya usajili wa majengo hayo sambamba na kutoa elimu ya namna bora ya uhifadhi wa bidhaa pamoja na kuhakikisha majengo yao yamekidhi vigezo vinavyohitajika.
"Sambamba na usajili na ukaguzi wa majengo na bidhaa za chakula na vipodozi, tunawasihi wenye maduka wanakagua mara kwa mara bidhaa zao ili kuhakikisha wanauza bidhaa ambazo hazijakwisha muda wa matumizi lakini pia wahifadhi vizuri bidhaa zao sehemu ambazo ni safi na salama" alisema Bw. Kahabi.
Kwa upande wake Afisa Masoko wa TBS Bi. Deborah Haule ametoa wito kwa wafanyabiashara wa chakula na majengo kusajili majengo yao katika mfumo ili kuepuka usumbufu wanaoweza kuupata pindi wakaguzi watakapopita katika maeneo yao.
"Usajili unafanyika kwa njia ya kielektroniki ukiingia katika tovuti ya TBS na kwenda katika huduma mtandao unaweza kujisajili wakati wowote na mahali popote, unatakiwa kuwa na TIN pamoja na leseni ya biashara ili kukamilisha usajili ". Alisema Bi. Deborah.
Majukumu haya ya usajili wa majengo ya chakula na vipodozi yalikasimishwa rasmi kwa TBS Juni 2019 ambapo hapo awali yalikua yakifanywa na iliyokuwa na TFDA.
Maafisa wa TBS wakiwasisitiza wamiliki wa majengo ya biashara ya chakula na vipodozi wa Halmashauri ya Mlimba, Morogoro kuhakikisha wanatoa huduma katika maeneo safi na salama pamoja na kuuza bidhaa ambazo hazijakwisha muda wa matumizi ili kulinda afya za watumiaji.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment