ZANZIBAR YAADHIMISHO SIKU YA MALARIA DUNIANI | Tarimo Blog

 Na Ramadhani Ali - Maelezo       

Imeelezwa kuwa kiwango cha maradhi ya Malaria Zanzibar sio cha kutisha lakini juhudi zaidi zinahitajika kuhakikisha lengo la kuyaondosha kabisa maradhi hayo linafikiwa.   

Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrisa Kitwana alieleza hayo katika maadhimisho ya siku ya Malaria Duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni.

Amekumbusha kwamba mwaka uliopita watu 20 waliripotiwa kufariki dunia kutokana na kuugua maradhi ya malaria hali inayoonyesha kuwa bado maradhi yaho yapo Zanzibar.

Alieleza kuwa suala la kuimarisha usafi wa mazingira, kuondosha mazalio ya mbu, matumizi sahihi ya vyandarua vilivyotiwa dawa na kupiga dawa sehemu ambazo  maradhi hayo yanaendelea kujitokeza ni miongoni mwa mikakati ya kuondosha kabisa.

Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Mjini Mgharibi alisema takwimu zinaonyesha wagonjwa wengi waliougua malaria katika miaka ya karibu ni waliotoka nje ya Zanzibar ama wenye tabia ya kusafiri mara kwa mara.

Amewashauri wananchi watakaojihisi wanadalili za kuugua malaria kuwahi vituo vya afya kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu ili yasiweze kusambaa zaidi kwa wananchi wengine.

Akitoa salamu za Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Mwakilishi Mkaazi wa Shirika hilo Zanzibar  Dk. Ghirmany Andermaechal amesema maradhi ya Malaria yanaendelea kuwasumbua wananchi wengi katika Bara hilo na kupelekea vifo vingi.

Ametaka mashirikiano ya pamoja baina ya wananchi, wadau mbali mbali na mashirika ya Kimataifa katika kukabiliana na maradhi hayo ili kuhakikisha hayasumbui wananchi.

Kaulimbiu ya siku ya Malaria Duniani mwaka huu ‘Tumia chandarua kilichotiwa dawa kitatukinga na Malaria.

Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrisa Kitwana awataka wananchi kuongeza juhudi ya kumaliza malaria Zanzibar katika maadhimisho ya siku Malaria duniani yaliyofanyika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni.
Mwakilishi Mkaazi wa WHO Zanzibar Dk. Ghrimany Andermichael akitoa salamu za Mkurugenzi Mkuu wa Shirika Hilo Barani Afrika katika maadhimisho ya siku ya Malaria Duniani yaliyofanyika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni.
Baadhi ya wafanyakazi wa Wizara ya Afya na wageni waalikwa walioshiriki maadhimisho ya siku ya Malaria Duniani wakimsikiliza Mkuu wa mkoa Mjini Magharibi (haypo pichani) katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni.
Mkuu wa Mkoa Mjini Mgharibi Idrisa Kitwana akimkabidhi cheti Mkurugenzi Msaidizi Afya, Manispaa ya Mjini Ramadhani Mikidadi kwa kushinda nafasi ya kwanza katika mashindano ya usafi na afya.
Picha ya pamoja ya mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya Malaria Duniani, Idrisa Kitwana (watano kulia) na viongozi wa Taasisi mbali mbali za Afya baada ya kukamilika maadhimisho hayo katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni.

Picha na Mkame Mshenga

 


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2