Na Mwandishi Wetu, Dodoma
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka kimesema kwamba kinaridhishwa na juhudi za kisera zitokanazo na ufanisi, upeo na maarifa alionayo Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika medani za Kimataifa katika Utekelezaji wa Sera ya Nje na kuimarisha Sera ya Diplomasia ya Kiuchumi
Hayo yamesemwa na Chama hicho baada ya Rais Samia kufanya ziara nchini Kenya na kisha kupata fursa ya kuhutubia mabunge mawili ya nchi hiyo.
Akizungumza jijini Dodoma, Shaka amesema, Rais Samia licha ya kuonesha upeo, maarifa na ufahamu mpana wa masuala ya Kidiplomasia, ameweka bayana msimamo wa nchi yake akionesha dhamira njema ya kutaka uendelezwa ushirikiano wa Kanda ya Afrika Mashariki.
Ameongeza CCM haikukosea kumteua kuwa Mwenyekiti wa Chama, kwani Chama chake hakikuwa na hofu katika kushika nafasi hiyo nyeti na ya juu kabisa kutokana na uzoefu na umahiri wake wa Uongozi.
" Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania ni kuendeleza diplomasia ya kiuchumi baada ya kupata mafanikio makubwa ya kujitangaza, kuweka bayana misimamo yake hatimaye kufahamika kimataifa kutokea awamu ya kwanza hadi ya sita.Rais Samia amekuwa ni Rais wa awamu ya sita.
"Amekuta wakuu wenzake wa nchi wakiwa madarakani hivyo hana budi kuwatembelea, kujitambusha, kujadiliana na kuendeleza na kuboresha mambo yote mazuri yaliofanywa na mtangulizi wake, Hayati Dkt. John Magufuli.
"Rais hatazuiwa kwenda mahali popote kwakuwa zipo sababu maalum kwa maendeleo ya nchi na watu wake. Hatasita kushiriki kwenye meza za majadiliano ya kisiasa au ya kiuchumi,. Atashiriki mazugumzo ya kibiashara, uwekezaji na mijadala ya kilimo afya, mazingira na mabadiliko ya tabia nchi . " amesisitiza Shaka.
Ameongeza Rais Samia katika hotuba yake ameweka bayana haja ya kuvutia wawekezaji, Kama ilivyoahidiwa na CCM katika Ilani ya Uchaguzi 2020 – 2025 Fungu la 22 (a) “Chama kitazielekeza serikasli zake mbili, Kuimarisha Utekelezaji wa Mpangpo wa kuboresha mazingira ya Biashara na Uwekezaji Nchini ili kuendelea kuvutia Sekta Binafsi kushiriki katika uwekezaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuiweka nchi katika nafasi nzuri katika mizania ya kimataifa ya wepesi wa kufanya biashara.”
Shaka amefafanua kuwa, ziara hiyo ya Mhe. Rais ni utekelezaji wa Ilani ya CCM katika masuala ya Kidipomasia na kusisitiza kuwa, katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020 – 2025 Fungu la 132 (a ) inaeleza,
“Chama kitaielekeza Serikali, kuboresha utekelezaji wa mipango ya kuimarisha diplomasia ya siasa ya kimkakati kwa ajili ya kulinda amani, uhuru, maslahi ya Taifa na kuimarisha ujirani mwema pamoja na kushiriki kikamilifu katika kuimarisha utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kukuza mahusiano ya kiuchumi na Mataifa, Jumuiya za Kikanda na taasisi nyingine za Kimataifa.”
Aidha, Chama kimempongeza Rais Samia, kwa kuendeleza msisitizo kwa kuyapa msukumo masuala ya ulinzi na usalama, mapambano dhidi covid 19 pia ushirikiano wa vyombo vya ulinzi na usalama wa kikanda na katika kukabiliana na uhalifu. .
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment