CCM WAMLILIA TEDDY MAPUNDA, WAUKUMBUKA WEMA NA MCHANGO WAKE WA KWA MAENDELEO YA TAIFA LA TANZANIA | Tarimo Blog


Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi( CCM) Shaka Hamdu Shaka akitoa heshima zake za mwisho kwa marehemu Teddy Hello Mapunda aliyefariki dunia Jumamosi ya wiki iliyopita.

Matukio mbalimbali katika picha wakati wa maziko ya marehemu Teddy Hello Mapunda aliyefariki dunia hivi karibuni.
Shaka Hamdu Shaka ambaye ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) akisalimia waombolezaji wakiwemo wana familia ya marehemu Teddy Hello Mapunda.


Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV

CHAMA  Cha Mapinduzi (CCM), kimemtaja marehemu Magdalena Theresia (Teddy) Hollo Mapunda kuwa ni mdau muhimu na mshirika kinara wa shughuli za maendeleo ya Taifa la Tanzania ambapo wakati wa uhai wake alishirikiana vyema na Chama pamoja na Serikali kupitia tasnia ya habari. 

Hivyo Chama hicho kimesema Taifa  limempoteza Mtanzania makini aliyejengeka vyema katika misingi ya uzalendo na utaifa na kwamba marehemu Teddy atakumbukwa kwa tabia yake ya kupenda ucheshi, huruma na upendo akiwa si mwenye majivuno , asiyedharau wenzake lakini pia hakupenda kujikweza na kuwakoga watu.

Akizungumza na baadhi ya vyombo vya habari kabla ya mazishi kufanyika nyumbani kwa marehemu Mbezi Beach mkoani Dar es Salaam, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Daniel Chongolo amemtaja Teddy kuwa  alikuwa mtanzania aliyependa tasnia ya habari na kuhakikisha habari muhimu zinawafikia wananchi wanaoishi vijijini na mijini  kwa haraka na usahihi. 

Shaka amesema Teddy alikuwa na kiu na mbinu za uwezeshaji wa kutosha ili habari ziweze kuwafikia wananchi na kuitangaza nchi yake hasa alipokuwa akifanyakazi  katika mbuga ya wanyama ya Taifa Serengeti. 

"Marehemu Teddy sifa yake  kubwa ilikuwa ni unyenyekevu, ucheshi na  moyo wenye huruma. Alikuwa ni mtanzania mzalendo, mtaifa na mchapakazi aliyependa kuona umoja wa kitaifa ukidumu nchini,"amesema Shaka na kuongeza atakumbukwa kwa tabia yake na mwenendo bora na adilifu  kwani hakuwa mtu mbabaishaji,hakuwa mtu wa  kutotimiza miadi mnapowekeana  ahadi kwani aliheshimu wakati.  

"Tuige maisha  aliyoishi mwenzetu hapa duniani kwani hakuwa mtu wa majivuno. Hakuwa akivunja miadi pia hakupendelea wala kuwa na roho ya korosho. Mikono yake haikuwa kama ile ya birika, badala yake alipenda kuwasaidia wenzake kila alipoweza na kuitazama jamii,"amesema Shaka.

Aidha amesema ni watu wachache mno duniani pale wanaopata nafasi hujikuta wakizitumia vibaya kuwakomoa wenzao, kuwanyanyasa na kuwapuuza wengine jambo ambalo katika maisha ya Teddy ilikuwa ni kinyume  na hivyo. 

Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi amewahimiza  watu wengine kutambua kuwa wanadamu katika dunia wana  safari fupi  hivyo  isiwaghilibu badala yake kila mmoja ajijue  iko siku ataondoka duniani na kurudi kwenye vumbi.

Shaka amesema Chama Cha Mapinduzi kinatuma  salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu na kumuomba Mwenyezi Mungu awake familia, ndugu, jamaa na marafiki wa Teddy, subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu kwao cha  msiba na maombolezo na tunaungana na wafiwa wote kumuomba Mungu amuweke mahali pema peponi. 


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2