COSTECH YATAKIWA KUJENGA KITUO CHA UUNIFU BAGAMOYO | Tarimo Blog

Mkurugenzi Mkazi wa Mfuko wa Maendeleo ya Watu (HDIF), Joseph Manirakiza akizungumza wakati wa uzinduzi wa  maonesho ya saba ya wiki ya Ubunifu yaliyoanza leo Mei 17, 2021 jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa LAPF Kijitonyama, mkoani Dar es Salaam.
Naibu waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia,  Omary Kapanga, akizungumza wakati akifungua Maonesho ya wiki ya ubunifu leo Mei 17, 2021 katika kumbi za LAPF Kijitonyama, Dar es Salaam
Naibu waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia,  Omary Kapanga (wa katikati mbele) Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe ( kushoto), Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia  Dkt. Amos Nungu na wageni mbali mbali, wakifuatilia uzinduzi wa Maonesho ya wiki ya ubunifu leo Mei 17, 2021 katika kumbi za LAPF Kijitonyama, Dar es Salaam
Baadhi ya wafanyakazi wa HDIF wakifuatilia ufunguzi wa wiki ya ubunifu
SERIKALI  imesema iko katika hatua ya mwisho ya kufanya  mapitio ya sera ya sayansi na teknolojia ili kuendana na hali ya ubunifu wa kidigitali  na kuzifanya kuwa bidhaa zinazouzika.

Sera hiyo  itasaidia kuwaleta, kuwatambua wabunifu na kuwaendeleza ili waweze kuleta mabadiliko ya kidigitali. 

Aidha serikali  imeitaka Tume ya Sayansi na Teknolojia  (COSTECH ), kujenga kituo cha ubunifu  katika kijiji cha Bagamoyo  kitakachowakutanisha wabunifu na bunifu zao mbalimbal  ili watu waweze kujifunza namna ya kujiajiri pindi wanapomaliza masomo yao.

Kipanga amesema serikali  itahakikisha inaendelea  kuboresha mazingira ya biashara katika kuchangia  ukuaji wa uchumi kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa katika teknolojia na pia kuratibu, kusimamia na kuzifanya bunifu zote kuwa bidhaa na kwamba ni wakati wa wabunifu  hao kubuni vitu vyenye tija ili kutatua changamoto kwenye jamii.

Ameongeza kuwa, serikali pia itaendelea kuimarisha miundombinu  yote ya mawasiliano kwani mawasiliano yamekuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi,  Lakini serikali pekee haitaweza kuleta mabadiliko  ya hayo endapo hatutashirikisha wadau, wabunifu na wafadhili.

"Ubunifu umechangia katika kuongeza ajira kwani huduma nyingi zinatolewa kwa njia ya mtandao  ikiweko ulipaji wa bili mbalimbali ikiwemo maji, umeme na leseni za biashara na hata kutuma pesa kwenda umbali wowote.

Naye Mkurugenzi  Mkazi wa HDIF Joseph Manirakiza amesema, mpango wa Maendeleo wa miaka mitano umeelezea umuhimu wa kukuza ubunifu na teknolojia  katika kuongeza  uzalishaji  na kutoa nafasi katika kuchangia ukuaji wa uchumi kidigitali.

Amesema tangu kuanzishwa kwa mradi huo miaka saba iliyopita HDIF imechangia ukuaji wa masuala ya ubunifu nchini ambapo mpaka sasa imeishafadhili miradi 48 kutoka kwa wabunifu wadogo 55 na atimizi kupitia mashindano kwa kushirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).

"Tunajivunia mafanikio makubwa ya kuibua wabunifu na kuifanya wiki hii kuwa kubwa ambapo sasa serikali kupitia Waziri Mkuu ametutaka wiki ya ubunifu iwe inafanyika kila mwaka kuanzia ngazi ya Mkoa Wilaya hadi taifa na mwaka huu mbali na Dar es Salaam mikoa mingine yanakofanyika maonyesho hayo ni, Arusha, Zanzibar, Morogoro, Iringa, Mbeya, Mwanza na Tanga.

Hivi karibuni Rais wa Jamuhuri  ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu alisema dunia ipo katika  Mapinduzi ya nne ya viwanda na kwamba uchumi wake unategemea teknolojia, Tanzania haiwezi kubaki nyuma katika kuwekeza katika sekta hiyo ya kidigitali kama utakumbuka wakati wa corona shule chache ndizo zilikuwa zinaendelea kutoa elimu wakati shule zilipofungwa na ni kwa sababu waliwekeza katika teknolojia hiyo ya kisasa iliyoibuliwa na ubunifu. 

"Tumefanya kazi pamoja na serikali  kupitia Costech  na wakati mwingine  wizara  lengo likiwa kubadilishana  uzoefu na uelewa. Tumewasaidia Costech katika kuwasaidia wabunifu na watafiti lakini ubunifu Tanzania  bado unahitaji fedha, kuwajengea wabunifu uelewa  na  kuweka  mazingira wezeshi kwa  kuboresha  sera".

Alisema wamekuwa wakitoa fedha na masuala ya kiufundi katika  bunifu zinazogusa sekta za maji, afya na elimu na kuchangia kuimarisha ubunifu katika kutatua changamoto  katika  jamii. 

Aidha Manirakiza amewataka wabunifu kuhakikisha wanaendelea kubuni vitu vyenye kutatua changamoto  kwa jamii na kwa upande wa  serikali kuendeleza mfumo huo katika  kuongeza  uzalishaji, kufanya  mapitio ya sera ili kukuza teknolojia na wafadhili  waendelee kushirikiana na serikali kuhakikisha ubunifu unakua nchini.

Wiki hiyo ya Ubunifu nchini imeandaliwa na Mfuko wa Ubunifu kwa Maendeleo ya Binadamu (HDIF) kwa kushirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia ( COSTECH)  pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP). 

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2