Na Mwandishi Wetu
WAKALA wa Mabasi Yaendayo Haraka DART kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama Barabarani, wameanza operesheni maalum ya kukamata wanaopita kwenye Barabara za Mabasi Yaendayo Haraka, wakiwemo waendesha Bodaboda, Bajaji, magari binafsi pamoja na magari ya serikali na yale ya majeshi mbalimbali.
Akizungumza katika zoezi la ukamataji wa madereva wanaopita kwenye barabara za Mabasi Yaendayo Haraka eneo la Kinondoni Mwanamboka mkoani Dar es Salaam, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Dumu Mwalugenge kutoka Makao Makuu ya Polisi kikosi cha Usalama Barabarani amesema zoezi hilo ni endelevu na linalenga kukomesha vitendo vya uvunjifu wa sheria vinavyofanywa na baadhi ya wananachi wasiotaka kutii sheria bila shuruti.
“Unaona baadhi ya madereva wa pikipiki wakiwa wamekamatwa , hii ni kuonyesha msisitizo kwamba lazima sheria zifuatwe na kusiwe na ulazima wa kutumia nguvu mara kwa mara, kwani jamii iliyostaarabika inafuata sheria kanuni na taratibu zilizowekwa ili kuzuia ajali za mara kwamara zinazoendelea kujitokeza kwenye barabara za Mabasi Yaendayo Haraka.
Mkaguzi Mwalugenge amesema barabara hizo zimejengwa mahsusi kwaajili ya Mabasi ndio maana hata ukiziangalia vizuri michoro yake chini kwenye sakafu za barabara imendikwa “Bus” hivyo ni pekee kwaajili ya mabasi na sio boda boda, bajaji wala magari binafsi na hata ya Serikali.
Aidha amesema madereva wa magari ya Serikali ndio wanaongoza kwa kuvunja sheria hasa kupitisha magari kwenye barabara za Mabasi Yaendayo Haraka, hivyo akatoa wito kwa wale wenye tabia hiyo kuacha mara moja kwani sheria haiangalii kazi wala cheo cha mtu yeyote atakayekiuka atashughulikiwa ikiwemo kukamatwa na kupelekwa mahakamani.
“Madereva wa Serikali hawako juu ya Sheria natoa onyo waendelee kutii sheria bila shuruti ndiomaana unaona operesheni hii inayoambatana na kutoa Elimu ya matumizi sahihi ya barabara za Mabasi Yaendayo Haraka inaendelea” Alisema.
Katika zoezi hilo ambalo Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wanatoa elimu ya matumizi sahihi ya Barabara za Mabasi Yaendayo Haraka, ili kusaidia kupunguza ajali za mara kwa mara zinazosababishwa na matumizi yasiyofaa ya miundombinu hiyo.
Miongoni mwa matumizi yasiyofaa ya Barabara za Mabasi Yaendayo Haraka ni pamoja na kupitisha magari binafsi na ya Serikali katika barabara hizo, kupitisha pikipiki pamoja na Bajaji, kuvuka maeneo ambayo hayana vivuko vya waenda kwa miguu pamoja na pikipiki bajaji na vyombo vingine vya moto pamoja na vyombo baridi kama baiskeli na maguta kuvuka kwenye vivuko vya waenda kwa miguu wakiwa wanaendesha badala ya kuvikokota.
Hivi karibuni ajali nyingi zimetokea kwenye mfumo wa barabara za Mabasi Yaendayo Haraka zikihusisha pikipiki, na magari binafsi jambo ambalo linaongeza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa watumiaji wa barabara hizo, lakini pia kwa waenda kwa miguu.
Zoezi la kutoa Elimu kwa watumiaji wa barabara za Mabasi Yaendayo Haraka ni zoezi endelevu ambalo Wakala kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wanafanya kwa ajili ya kupunguza ajali lakini pia kuelimisha umma juu ya matumizi sahihi ya barabara pamoja na miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka ambayo ni vituo, barabara, madaraja ya waenda kwa miguu, pamoja na vivuko vya waenda kwa miguu.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment