DKT. GWAJIMA AFANYA UFUATILIAJI WA MUONGOZO NAMBA 7 WA USHAURI WA WASAFIRI KIA | Tarimo Blog

Na.Catherine Sungura, WAMJW-Kilimanjaro

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima, leo ametembelea uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) ikiwa ni kufuatilia utekelezaji wa muongozo namba 7 wa ushauri wa wasafiri wanaoingia nchini uliotolewa tarehe 4 Mei, 2021.

Katika muongozo huo moja ya maelekezo ni kufanya uchunguzi wa COVID-19 kwa kuwapima kipimo cha haraka (Rapid Test) wasafiri wote wanaoingia nchini, kwani kumekuwa na malalamiko kadhaa kutoka kwa wananchi kuhusu zoezi hilo. Mojawapo ya malalamiko hayo ni abiria kuchelewa kumaliza hatua za huduma ya vipimo vya afya.

Mhe. Waziri amebaini kuwa watumishi wapo na wanafanya kazi zao vizuri wakiwemo maafisa afya, maabara na watumishi wa uwanja wa ndege. Waziri amewapongeza watumishi hao kwa kazi nzuri wanaoifanya. Aidha, amewashukuru viongozi wa mkoa wa Kilimanjarao na Halmashauri ya Hai, Moshi kwa kutoa watumishi wa ziada ili kuongeza nguvu.

Amesema kuwa abiria kuchelewa kumaliza hatua za vipimo vya afya pia inachangiwa na baadhi yao kutojaza taarifa zao za hali yao ya afya kupitia mfumo wa kieletroniki wa afyamsafiri ambao unamtaka abiria kujaza taarifa zake ndani ya masaa 24 kabla ya kuingia nchini na hivyo kuwafanya wachelewe kuanza hatua ya uchunguzi wa awali (primary screening) na mwisho kufanya hatua zote za kulipia na kupima kuchelewa pia.

Aidha, ametoa wito kwa mashirika ya ndege na mamlaka ya viwanja vya ndege, usafiri wa ndege na wakala wa ndege, mabasi kushirikiana kutoa elimu ili taarifa hizo zijazwe mapema kabla ya kufika katika maeneo yetu ya viwanja vya ndege, bandari na mipaka yote.

Kwa upande wa vipimo vya awali ameelekeza ufanyike utaratibu wa kuongeza idadi ya wapimaji kutoka watano hadi kufikia 8 na wakati huo uratibu ufanyike kuomba wahasibu kutoka wizara ya fedha kwa ajili ya kuratibu malipo kwa ushirikiano na banki husika na wataalamu wa afya wahusike na kuongeza nguvu ya kutoa huduma za afya.

Pia kwa kuzingatia kuelekea msimu wa wageni wengi wizara itashirikiana na wadau wake kuimarisha huduma za vipimo vya haraka huku ikiendelea kupokea maoni mbalimbali na kuyafanyia kazi. Vilevile, amesema wizara itaendelea kuboresha mfumo wa afyamsafiri ili uweze kurahisisha taratibu za kuwahudumia wasafiri kabla hawajaanza safari na kupunguza changamoto mbalimbali wanazolalamikia wakati wanapowasili nchini.

Waziri wa Afya Dkt.Dorothy Gwajima akiangalia utaratibu wa uchunguzi wa awali wa Hali ya afya za wasafiri (Primary health screening) Katika uwanja huo

Waziri Dkt.Gwajima akimpima joto msafiri aliyewasili nchini ikiwa ni hatua za awali za uchunguzi wa Afya za wasafiri.

Eneo maalum la kupima kipimo Cha haraka Cha Covid-19 (Rapid Test) kilichopo ndani ya uwanja wa ndege wa KIA ambapo wasafiri wanaowasili nchini hupimwa kabla ya kuanza taratibu zingine ndani ya uwanja
Mmoja wa wataam wa Afya waliopo Kwenye vyumba maalumu vya kupima kipimo Cha haraka Cha Corona akipima kipimo Cha haraka Cha Corona kutoka kwa msafiri aliyewasili nchini.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2